Thursday, November 8, 2012

UA



UA unapochanua, wengi wanakuzengea,

Kila mtu na yake nia, na wewe hautoijua,

Mashairi hukwimbia, marashi yaliyotiwa,

Ua waringia nini, huchumwa kutiwa ndani ?



Hukupamba kwa ridhaa, ukawaka kama taa,

Huchumwa kwenye sinia, birikani kwenda tiwa,

Maji wakakumwagia, ubatizo ukapewa,

Ua waringia nini, kunesa hufika mwisho ?



Bustanini ukiwa, wanesa kwa kutulia,

Upepo kuuringia, na kuihofu mvua,

Uzuri ukaringia, usije kukupotea,

Ua waringia nini, kunesa hufika mwisho ?



Nyuki huwashangaa, kwa wingi kukuvamia,

Utamu ulojaliwa, wakawa waudokoa,

Wakenda jitengezea, kitamu usichojua,

Ua waringia nini, kumbe huwa wanyauka ?



Washtiri hukutwaa, wakenda kujiuzia,

Watu wakakunua, zawadi upate kuwa,

Kisha kuwapelekea, wazuri na wasokuwa,

Ua waringia nini, kumbe huwa wachakaa ?



Kisha kuwapelekea, wazuri na wasokuwa,

Wagonjwa na walofiwa, wote kupata hidaya,

Kumbukumbu kurejea, kumbe nao wahesabiwa,

Ua waringia nini, kumbe hupoteza rangi ?



Harufu hukusambaa, jasmini kawa wawa,

Na waridi la ulua, chuoni ulozaliwa,

Watu wakakusikia, hata kwa mbali ukiwa,

Ua waringia nini, kumbe huwa wachakaa ?



Waume hukutezea, kama picha vile kuwa,

Mashindano kuwatia, wala haya kutojua,

Muumbwa kwenda sifiwa, huwa kweli ajiumbua,

Ua waringia nini, kumbe huwa wachakaa ?



Sifa anayetakiwa, Muumba aliyekuwa,

Yako kukuzidishia, na salama kuipewa,

Usije kuadhiriwa, ikakucheka dunia,

Ua waringia nini, kumbe huwa wachakaa ?



Ila ninachoshangaa, shukurani kutotoa,

Hudhani umezaliwa, wala kuumbwa hukuwa,

Moto ukapalilia, kasri milelel kukaa,

Ua waringia nini, kumbe harufu hukoma ?



Ujana ukipangua, na maungo kupungua,

Tetracycline ukawa, na makengeza ukawa,

Washikaji hukimbia, wengine kwenda epua,

Ua waringia nini, kumbe huwa wazeeka ?



Mvuto ukipotea, nyuki wanakukimbia,

Huhamia palo poa, hai wakajisikia,

Jinai kwao ikawa, wewe kukutembelea,

Ua waringia nini, nyuki huwa wakususa ?



Ujana wala si saa, muda hautotimia,

Kwa wepesi hukimbia, kama radi ilokuwa,

Kufumba na kufumbua, uzee umeingia,

Ua waringia nini, kumbe mvuto huisha ?



Uzuri ukafifia, na mwisho ukapotea,

Kioo ukakimbia, na maji kukupembua,

Ikawa huna staha, ila raha na karaha,

Ua waringia nini, kumbe huwa wakauka ?



Laiti ungejijua, ua utajiangalia,

Muda ukautumia, ya kwako kujijengea,

Na mazuri kuyazua, kizazi kuja kufaa,

Ua waringia nini, hubakia historia ?

<<>>


No comments: