Friday, November 9, 2012

MAMBO Jambo TUMBO

SISIMIZI hadi tembo, maisha mambo ya tumbo,

Ya ndani hadi ya ng'ambo, hili halina vijambo,

Na nchi huenda kombo, haya yakiwa ya kambo,

Tunaishi kwa matumbo, hatuishi kwa mapambo !

Watu hawali mapambo, vineno na vijigambo,

Pasi funguo za tumbo, chaenda mrama chombo,

Kofuliye ya mgambo, hufunguka penye chambo,

Tunaishi kwa matumbo, hatuishi kwa mapambo !

Vigelegele na tambo, huwa havina ulimbo,

Huwa la mjinga fumbo, wala havina urembo,

Huwa halijali umbo, ila kazi za mtambo,

Tunaishi kwa matumbo, hatuishi kwa mapambo !

Watu huzirusha fimbo, yakipagawa matumbo,

Palipokuwa na nyimbo, pakazuka mitarimbo,

Na hakipiti kitambo, vilio vikawa ng'ambo,

Tunaishi kwa matumbo, hatuishi kwa mapambo !

Watu hawali mapambo, chakula ndoa ya tumbo,

Vinywaji ni vyake wimbo, kwa wilaya na majimbo,

Na matawi si malambo, kuna nyasi za machimbo,

Tunaishi kwa matumbo, hatuishi kwa mapambo !

Kuna mifuko ya tembo, hutafuta tupu tumbo,

Njaa ikawa ni chambo, ndani kutiwa mkumbo,

Ukaufuata wimbo, kwako usio na lambo,

Tunaishi kwa matumbo, hatuishi kwa mapambo !

Rushwa kwao ni nembo, na kaisha pia msimbo,

Yao ukifanya lambo, kwa papo huwa ulimbo,

Ukawa katika chimbo, la kuwafaa wadambo,

Tunaishi kwa matumbo, hatuishi kwa mapambo !

Ya jibini na ya kimbo, huwa haviendi mwambo,

Wameeleka msimbo, toka zama za maumbo,

Anayajua Chilambo, enzi hizo za Urambo,

Tunaishi kwa matumbo, hatuishi kwa mapambo !

Ayakubali Kalembo, toka shimo la vikumbo,

Chuoni kwenye majambo, Harry alitia nembo,

Leo si mtu wa Mombo, Mnyakyusa si Mnyambo,

Tunaishi kwa matumbo, hatuishi kwa mapambo !

Wameona kina Ndimbo, na iliyobaki shombo,

Haijakuwa urembo, ukashibisha matumbo,

Dunia hii ya jambo, huwa likazua jambo,

Tunaishi kwa matumbo, hatuishi kwa mapambo !

Hata akiwa ni Rambo, halifai tupu tumbo,

Atajioa isembo, akavishindwa vikumbo,

Ila likishiba tumbo, hapo huwa mtarimbo,

Tunaishi kwa matumbo, hatuishi kwa mapambo !

Yakishashiba matumbo, fani huwa ndio nyimbo,

Yakapendeza marembo, na yakang'ara mapambo,

Huwa chateleza chombo, hata kama cha miombo,

Kuna mifuko ya tembo, hutafuta tupu tumbo,

Njaa ikawa ni chambo, ndani kutiwa mkumbo,

Ukaufuata wimbo, kwako usio na lambo,

Tunaishi kwa matumbo, hatuishi kwa mapambo !

Rushwa kwao ni nembo, na kaisha pia msimbo,

Yao ukifanya lambo, kwa papo huwa ulimbo,

Ukawa katika chimbo, la kuwafaa wadambo,

Tunaishi kwa matumbo, hatuishi kwa mapambo !

Kawaulize Warombo, pundamlia msombo,

Wana mikubwa mitambo, humfukuza kijimbo,

Mwenye mimba kenda kombo, mwana huwa chaurembo,

Tunaishi kwa matumbo, hatuishi kwa mapambo !

Mwenzenu ningali mwambo, njaa ni yangu wimbo,

Sijaona wa miyambo, kuja lihifadhi tumbo,

Ushairi zangu tambo, kwangu mambo jambo tumbo,

Tunaishi kwa matumbo, hatuishi kwa mapambo !

No comments: