Wednesday, November 14, 2012

KATIKATI NITAPITA


Njia wakinifungia, katikati hupitia,

Misitu hujifekea, uwazi kujipatia,

Na milima hupangua, safari kuendela,

Katikati nitapita, na wala hutoniona!



Weledi huwaachia, wajuao wasojua,

Langu nikiliamua, nuru yanitangulia,

Na mtu sijamlilia, wala ya kumtegemea,

Katikati nitapita, na wala hutoniona!



Nilithubutu tamaa, mtu nikamtegemea,

Muda sikumalizia, kiumbe nikamjua,

Uungu keshanunua, ataka kuabudiwa,

Katikati nitapita, na wala hutoniona!



Ndipo nikayaachia, mkiwa nikabakia,

Na huku sio kulia, ila kujihurumia,

Mola ninamrejea, na yake kukumbatia,

Katikati nitapita, na wala hutoniona!



Ndiye wa kunijalia, waja nikawaachia,

Yao niliyoyachukua, nipare warudhishiwa,

Na utunzi maridhia, kwalo hilo nanuia,

Katikati nitapita, na wala hutoniona!

No comments: