Thursday, November 8, 2012

Kila mnachoamua


WENGI ninavyowajua, watasema upuuzi,

Rai wakaikataa, na kuniona mshenzi,

Mimi ninalojua, dhikiri tayari mtenzi,

Kila unaloamua, ni thawabu au dhambi !



Siku ikijawadia, nina la kujitetea,

Langu niliwaambia, hamkuwa wa kusikia,

Changu chema 'meachiwa, sintouona udhia,

Kila unaloamua, ni thawabu au dhambi !



Mtu hakuninunua, wala sijawanunua,

Sikutumia rupia, ukubwa kuugombea,

Na ngazi sikutumiwa, waovu kujipandia,

Kila unaloamua, ni thawabu au dhambi !



Haramu sikutumia, miye nilikikataa,

Wala siri haikuwa, na nyie niliwaambia,

Ila kwa kuipenda dunia, mlitanguliza tamaa,

Kila unaloamua, ni thawabu au dhambi !



Kizazi hamkuwazia, utumwani kitakuwa,

Kwa uchu mlichukua, visenti kuvitumia,

Nchi mkajiuzia, bila ya kujitambua,

Kila unaloamua, ni thawabu au dhambi !



Wa umoja wakuua, rafiki mkachagua,

Mwalimu alokataa, nyie mkakiridhia,

Gunzi sikio kutia, Nyerere kutomsikia,

Kila unaloamua, ni thawabu au dhambi !



Mbali hamkuangalia, mkaiangukia pua,

Njaa iliyowasumbua, amani kushambulia,

Na utulivu kuvia, nchi ikaumbuliwa,

Kila unaloamua, ni thawabu au dhambi !



Yafaa kujipimia, wapi pa kusimamia,

Waliotutangulia, daima huwa wajua,

Lipi la kulichagua, na lipi la kukataa,

Kila unaloamua, ni thawabu au dhambi !



Mzaha mkifanyia, mtakuja lijutia,

Majuto baba hajawa, sikuzote mwana huwa,

Na ndivyo itavyokuwa, siku itapowadia,

Kila unaloamua, ni thawabu au dhambi !



No comments: