Wednesday, November 14, 2012

Sura za televisheni -2


IMEKUWA yumkini,sasa kwao ofisini,

Wanayagawa mapeni, kucha wajae kiooni,

Msipowakosa machoni, watabakia moyoni,

Sura za televisheni, wananchi ziogopeni !



Hatuwaoni shambani, hiyo kazi ya maskini,

Ni watu wa vijijini, kuteseka maishani,

Hiyo ndiyo yao shani, hawawezi ya mjini,

Sura za televisheni, nyuma zina uzaini !



Chini hawana thamani, ameamua manani,

Wao watafanya nini, kuwapandisha uzani ?

Na sura zao si shani, kwonyesha televisheni,

Sura za televisheni, uongo sera yamini !



Huwaoni machungani, ila ni televisheni,

Kishake magazetini, wakkitoa auni,

Wenye njaa wathamini, walioficha bilioni,

Sura za matangazoni, huwa zanunua nini !



Hawaendi baharini, huko sawa machakani,

Tena ni mashenzini, miji ya Uswahilini,

Riziki ya mtihani, kwa wenye elimu duni,

Sura za machapishoni, zinauza kitu gani !



Habari ni yao nuni, haifai masikini,

Mkakati wao kuni, na moshi mkali machoni,

Maisha ya vijijini, nani anayathamini ?

Sura za televisheni, zingine za mumiani !



Zinawekwa mafichoni, hatuoni uwanjani,

Mkitia hesabuni, jibu lake katoeni,

Wa shule sio chuoni, ubishi wako wa nini ?

Sura za taarifani, zinamlaghai nani !



Umma msiziamini, wanadhamini utani,

Kiilo kwao huwa tani, waseme wamewapeni,

Huwa wauza hisani, na haitoki rohoni,

Sera zza televisheni, umma msiziamini !



Kiini mtathmini, vilivyopo gazetini,

Kuna mengine dukani, yatangaza udhamini,

Yanunuliwa kwa tini, hayajali bwana gani,

Sera za magazetini, kiini mtathmini!



Wakwaza utamaduni, kuthamini vya kigeni,

Na nchi iko shakani, kizazi wanakihini,

Tutavizaa vigeni, visikalike nchini,

Sura za utamaduni, hivi huwa ni wa nani !



Yakini ichungueni, wasemayo mkutanoni,

Mengi yao ya kihuni, si fursa kuwapeni,

Matatizo wachiani, aje amalize nani ?

Sura za mtandaoni, yakini angalieni !



Kuna wengine shetani, hata pia mumiani,

Vampaya waitwani, 'dracula' adhamini,

Wanafurika nchini, wa nje pia wa ndani,

Sura zitakazo shani, anazipenda shetani !



Hubadilika gizani, wakayeyuka nuruni,

Huishi majenezani, hadi usiku wa manani,

Mbalamwezi huadhini, ya kwao misikitini,

Sura za mikutanoni, maswala ziulizeni !



Hupigania yamini, uzazi wake amani,

Hali hawana moyoni, ila wanayoyatamani,

Huachia usukani, kwa kutazama pembeni,

Sura za mahekaluni, kazipimeni amani!



Bidhaa kazijueni, ladha zichanganyeni,

Wajiuza watu gani, na mnunua ni nani ?

Kisha na huko sokoni, hivi kabakia nani?

Sura za maguioni, bidhaa kazijueni !



Wachungani chungueni, walozika ardhini,

Au kilicho hewani, kinachopaa angani,

Usijekuta motoni, ni papa hapa duniani,

Sura zenye mitihani, chungueni umakini !



Salama mtathmini, na kama mwayaamini,

Kuna wazushi nchini, waiweka mfukoni,

Kama h auna mapeni, vigumu kuiauni,

Sura za usalamani, salama katathminini !



Pitieni vitabuni, sura za mahesabuni,

Udhinbiti watiani, ukaleta afueni,

Au wote wamo kundini, aliwaye masikini ?

Sura za mahesabuni, udhibiti kafanzeni



Sikillizeni uani, yaimbwayo akilini,

Nani shida atamani, kama sio afkani,

Na wetu umajinuni, vipi watusaidiani ?

Sura humu vikaoni, sikizeni akilini !



Wajazanapo vitini, waila hesabu gani,

Na nafuu yao nini, walio madarakani,

Au twatumia tani, tukavuna nusu tani ?

Sura za utumishini, kutumwa kayaoneni !



Nimefika tamatini, kwangu hapo ni mwishoni,

Kuzidi sijatamani, nikabakia juani,

Mbegu nawaachieni, mtakako kapandeni,

Sura za taasinini, ukweli kaubaini !



No comments: