Sunday, November 18, 2012
ASIYETAKA K UKOSOLEWA
Nimeioina tabia, makosa wayakimbia,
Rushwa waliochukua, wakataa kuambiwa,
Kazi yao kuzomea, tumbo wakashtakia,
Asotaka kosolewa, hivi huyo mtu mzima ?
Hii ndiyo Tanzania, inakotawalal njaa,
Tumbo linanunuliwa, na akili kuzitoa,
Moyo wakautumia, haramu kuvichagua,
Asotaka kosolewa, hivi huyo mtu mzima ?
Kilio anayelia, kiungo ameungiwa,
Sura ukiangalia, watu utawadhania,
Nyuma ukichungulia, mkia unatokea,
Asotaka kosolewa, hivi huyo mtu mzima ?
Watu changa wawatia, machoni limeingia,
Hao hao walokuwa, tofauti wajitia,
Kuna wanalokusudia, na Mola analijua,
Asotaka kosolewa, hivi huyo mtu mzima ?
Akili mkifungua, siri mtaigundua,
Si wengine walokuwa, haohao mwawajua,
Roho wamezifulia, kulemaza Tanzania,
Asotaka kosolewa, hivi huyo mtu mzima ?
Nayo mkiyaachia, vijana kuangamia,
Zuri hamtoambua, balaa inawajia,
Hakika mkichelewa, ng'ombe wayo mwawauziwa,
Asotaka kosolewa, hivi huyo mtu mzima ?
Ng'ombe wayo mwauziwa, katu nchi haitakuwa,
Miti ikendazolewa, mkaa ukabakia,
Vito mkahujumiwa, na mashimo kubakia,
Asotaka kosolewa, hivi huyo mtu mzima ?
Kitu hamtajaliwa, bali dhiki na udhia,
Heri itawakimbia, shari kuwaingilia,
Akili msipotumia, wenyewe mtaumia,
Asotaka kosolewa, hivi huyo mtu mzima ?
Wachunguzi wanambia, mzungu wanaujua,
Nyumba imeshachafuliwa, na mto unatakiwa,
Maji yake kuingia, makazi safi yakawa,
Asotaka kosolewa, hivi huyo mtu mzima ?
Kazi kubwa itakuwa, mwaweza kuikimbia,
Ila isipozingatiwa, makubwa yatatokea,
Mkisimama radhia, dosari mtafagia,
Asotaka kosolewa, hivi huyo mtu mzima ?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment