Sunday, November 18, 2012

Usultani wautaka


Hamnao visiwani, sasa bara wabakia,

Kama vile ni utani, vyamani wajipandia,

Ingawa siliamini, ndilo linalotokea,

Usultani wautaka, waliokuwa hawana !



Umeisha visiwani, bara ndio waingia,

Wanaupanda maweni, na mafuta kumwagia,

Kila nikitathmini, ninashindwa kuelewa,

Usultani wautaka, waliokuwa hawana !



Huu ni uafkani, kitu gani inakuwa,

Kina nani majinuni, hali wasiyoijua,

Watumia dira gani, huku wanakoelekea ?

Usultani wautaka, waliokuwa hawana !



Seyyid Said ngamani, omoni kesharejea,

Kafufukia Omani, mjini akaingia,

Ila sio visiwani, Mrima ametulia,

Usultani wautaka, waliokuwa hawana !



Na wameanza kuhani, mzimu kuillilia,

Nywele zao kichwani, kalkiti wanatia,

Zipate kuwa laini, umanga kukurubia,

Usultani wautaka, waliokuwa hawana !



Weusi wauzaini, weupe kukimbilia,

Wajipaka vihinani, ngozi wakajichibua,

Weupe wapate winii, heshima juu kupaa,

Usultani wautaka, waliokuwa hawana !



Ya wengine si amini, huwa yansiginiwa,

Roho haziwi laini, kwao wasichokizaa,

Ila hutia imani, kwa sadaka kutoa,

Usultani wautaka, waliokuwa hawana !



Huibia masikini, wenye shibe wakapewa,

Wajumbe wakaamini, nchi watawagawia,

Wasiache usukani, daima kushikilia,

Usultani wautaka, waliokuwa hawana !



Wajivukiza ubani, na marashi kujitia,

Wakageuza peponi, hii ya kwao dunia,

Wanajua hawaioni, ya kweli iliyokuwa,

Usultani wautaka, waliokuwa hawana !



Walalao amesheni, sultani kumpokea,

Katokea ugenini, nyumbani anaingia,

Ameona kitu gani, bado mimi sijajua,

Usultani wautaka, waliokuwa hawana !



NgazI zao waamini, imara zilizokuwa,

Waanzia vijijini, na mjini wakatua,

Na kisha wilayani, kufikia wa mkoa,

Usultani wautaka, waliokuwa hawana !



Kisha huja taifani, makungi kujigawia,

Kuuenzi Usultani, kwenye mpya Tanzania,

Wanatafuta waghani, sasa waje wasifia,

Usultani wautaka, waliokuwa hawana !







No comments: