Thursday, November 8, 2012

Tujifunzeni Uchina


Umuhimu waujua, mkuu kumterua,

Huichunguza tabia, toka alipoanzia,

Kasoro huzikataa, mbali hawezi fikia,

Tujifunzeni Uchina, wachaguavyo rais !



Mwasisi aheshimiwa, Mao wanamtambua,

Mengi aliwausia, njia kutokupotea,

Ila aliowatia, labda upya kuzaliwa,

Tujifunzeni Uchina, wachaguavyo rais !



Kama jopo wanakaa, wengi kuwazungumzia,

Nini walichowafanzia, Wachina kuendelea,

Au baa kutatua, nafuu wakajipatia,

Tujifunzeni Uchina, wachaguavyo rais !



Tathmini hufanziwa, hakika iliyokuwa,

Ubora akajjua, na udhaifu kutambua,

Kunyoa akaamua, au kusuka ikawa,

Tujifunzeni Uchina, wachaguavyo rais !



Mazuri hupembuliwa, na mabaya kuambiwa,

Hisabu ikitimia, dhamana akaipewa,

Na malengo huwekea, kinyume hawezi kuwa,

Tujifunzeni Uchina, wachaguavyo rais !



Kumi anahesabiwa, cheoni kwena kukaa,

Wa sasa keshaambiwa, namba wani yatakiwa,

Uchina sasa ikawa, katika hii dunia,

Tujifunzeni Uchina, wachaguavyo rais !



Kazi si kushangilia, na vigelegele kutia,

Kazi huwa manufaa, watu wakajionea,

Vingine ikenda kuwa, ukaaji hupungua,

Tujifunzeni Uchina, wachaguavyo rais !



Pesa anayetumia, mwenyewe hujiondoa,

Hata watu 'kitumia, wenyewe humuumbua,

Wao wakamchongea, kitanzini kuingia,

Tujifunzeni Uchina, wachaguavyo rais !





No comments: