Sunday, November 18, 2012
MPITO
Ndivyo ilivyo dunia, wakati unafikia,
kwa nchi kujapitia, nafasi ya kujizaa,
Kamampya ikawa, au mbovu kuchakaa,
Kipindi hiki cha mpito, kazi kujilimbikizia !
Tumeacha ujamaa, ubepari twakumbatia,
Na mpito inakuwa, vya watu kuvichukua,
Kwa halali ya kuzua, na haramu ya kulea,
Kipindi hiki cha mpito, kazi kujilimbikizia !
Kiwewe wameingia, watu sasa kusifiwa,
Kwa ukubwa kuzidia, na fahari kuenea,
Kila mpenda dunia, yakini ni yake njia,
Kipindi hiki cha mpito, kazi kujilimbikizia !
Waililia dunia, udugu wakidhania,
Na milele watakaa, hawawezi kuugua,
Ila yawanyanyapaa, na wao hawajajua,
Kipindi hiki cha mpito, kazi kujilimbikizia !
Haiwapendi dunia, yawaona ni udhia,
Na hasa mnaokua, watukufu mmekua,
Kila siku inalia, lini mtaondolewa ?
Kipindi hiki cha mpito, kazi kujilimbikizia !
Yataka badilishiwa, wa heri ikapatiwa,
Si laana kuchukua, kitu isiyosaidia,
Muumba wamuambia, ni nini watufanyia ?
Kipindi hiki cha mpito, kazi kujilimbikizia !
Dhaifu twahitajia, dhalili waliokuwa,
Wanaokusujudia, na sifazo kuzitoa,
Hadi machozi kulia, kila wakikukumbukia ?
Kipindi hiki cha mpito, kazi kujilimbikizia !
Mizigo watuachia, kitu isiyotufaa,
Rabana twakulilia, hima kutupunguzia,
Mpito ukiishia, tuje wema kujaliwa,
Kipindi hiki cha mpito, kazi kujilimbikizia !
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment