Sunday, November 18, 2012

Wanaokula vya wezi



Swali nimelisikia, mjini lauliziwa,

Wezi wakishakwapua, mfukoni kuvitia,

Kisha wakakugawia, na wewe ukatumia,

Wanaokula vya wezi, hivi wao wezi pia ?



Japo wewe ulipewa, kwa nguvu hukuchukua,

Ni haramu yabakia, budi hilo kutambua,

Dhahiri ikishakuwa, kundini namo hutiwa,

Wanaokula vya wezi, hivi wao wezi pia ?



Halali haitakuwa, hicho ulichochukua,

Ni haramu hubakia, vingine haitakuwa,

Na madhambi wagawiwa, kama hilo hukujua,



Mama yahadhithiwa, vya mwana akipokea,

Wala hakuulizia, kule vinakotokewa,

Yeye akatamkiwa, mwana akamsifia,

Wanaokula vya wezi, hivi wao wezi pia ?



Akadai kwongezewa, utamu ulivyokolea,

Kasri akavamia, mwana vingi kuvitwaa,

Sultani kagundua, ndani mwana akatiwa,

Wanaokula vya wezi, hivi wao wezi pia ?



Hukumu haikuchelewa, kunyongwa kahukumiwa,

Mwana machozi kalia, mamaye kutokumlea,

Fursa alipopewa, kaomba mama kwitiwa,

Wanaokula vya wezi, hivi wao wezi pia ?



Mama alipoitiwa, kamwita kusogea,

Mama alipojongea, na sikio kumpatia,

Mwana akaliratua, kisiki kikabakia,

Wanaokula vya wezi, hivi wao wezi pia ?



Sababu aliyoitoa, ni mama kumuachia,

Wizi akaendelea, na vinono kufurahia,

Uchungu kamgawia, katika hii dunia,

Wanaokula vya wezi, hivi wao wezi pia ?

No comments: