Sunday, November 18, 2012

MJA KUDAI UHURU ...



Nani kasema makosa, mtu uhuru kudai,

Hata na wansiasa, hivi hili hawajui,

Kioja nakitomasa, ya rafiki na adui,

Mja uhuru kudai, hivi huwa ni makosa ?



Zama hizi za kunesa, rafiki huwa adui,

Pasina na kudodosa, mfu hugeuka hai,

Na hai ukamkosa, maiti kumsabahi,

Mja uhuru kudai, hivi huwa ni makosa ?



Maisha sio asusa, sio ndoa si nikahi,

Kuna saa na hamasa, na kutafuta uhai,

Wakati unapopasa, uhuru ni yako rai,

Mja uhuru kudai, hivi huwa ni makosa ?



Utumwa sio anasa, hali tu haizuii,

Dhiki ukishazitosa, usiwe hujitambui,

Hii swala sio misa, na wala si jinai,

Mja uhuru kudai, hivi huwa ni makosa ?



Kule na huku pepesa, kisha upate na rai,

Moyoni likikutesa, kulitoa si nishai,

Bali ndani ukisusa, moyo huwa hautulii,

Mja uhuru kudai, hivi huwa ni makosa ?



Maisha kupiga msasa, na kunoa maslahi,

Uso ukiupapasa, ikawa ni asubuhi,

Majini ukijitosa, hukurejea uhai,

Mja uhuru kudai, hivi huwa ni makosa ?



Kalipateni darasa, msiwe ni ndugu mui,

Msiozijua siasa, ila njaa kukinai,

Yapasayo kudodosa, dunia kutanabahi,

Mja uhuru kudai, hivi huwa ni makosa ?



Hii haijesha posa, wazazi hawatambui,

Yadaiwa kudodosa, zilizopo leo rai,

Ni bure kujitakasa, hali mchafu wajihi !

Mja uhuru kudai, hivi huwa ni makosa ?



No comments: