Sunday, November 18, 2012

Kumbe si hivyo wajinga

SIO watu wa kupinga, maguvu wakatumia,

Hawa watu wa kupanga, akili wakatumiya,

Kufungua na kufunga, hii ni yao tabia,

Wapole Watanzania, si kumbe hivyo wajinga !

Sio watu wa kuringa, wangalia hatua,

Sura sio za kuchonga, asili waichukua,

Hapa wameweka nanga, nani wa kuwaondoa ?

Wapole Watanzania, si kumbe hivyo wajinga !

Hawa watu wa kulenga, lengo wakakadiria,

Shabaha wakiinyonga, palepale kwenda kuwa,

Upinde hautapinga, tunduni kwenda ingia,

Wapole Watanzania, si kumbe hivyo wajinga !

Hawa waut wa kusonga, wajua kujipikia,

Ya kwao kutabananga, bila ngao wala gia,

Hawauhofu ukunga, mkubwa akiachia !

Wapole Watanzania, si kumbe hivyo wajinga !

Hawa watu wa kukonga, nyoyo ukawaridhia,

Maguvu ukiyapunga, mwenyewe hukurudia,

Nani wa kutangatanga, na nyumbani akujua,

Wapole Watanzania, si kumbe hivyo wajinga !

Katika ardhi na anga, asili tunaijua,

Visiwa hivi vyalonga, dini vilishaipewa,

Wageni wakitusonga, yetu hatutawaachia,

Wapole Watanzania, si kumbe hivyo wajinga !

Wanaotumwa ukunga, ukafiri kuuzaa,

Ndhimi zao wangechunga, na miili kuaangalia,

Wachamungu wanatanga, na Mola wamlilia,

Wapole Watanzania, si kumbe hivyo wajinga !

Imani hii kupinga, kiini wakichezea,

Huo mkubwa ushonga, hauwezi kubaliwa,

Ya kwenu kutangatanga, hayawezi chini tua,

Wapole Watanzania, si kumbe hivyo wajinga !

Kamba msipojiunga, wazi mkaiachia,

Wenyewe mnajinyonga, ni bora kujiondoa,

Twataka nchi kujenga, Mungu akafurahia,

Wapole Watanzania, si kumbe hivyo wajinga !

No comments: