Sunday, November 18, 2012

MIUNGU WATU


WALE na waitumie, waliokwishajaliwa,

Katu wasinihurumie, wala kuja nigawia,

Razaki nimjuae, yangu atanipatia,

Mola wanaojifanya, sitaki fadhila yao !



Ya kwao niwaachia, yangu nitajifanyia,

Pamwe na maruerue, wala siwezi sinzia,

Sintokihofu kiwewe, cha njaa na kuishiwa,

Mola wanaojifanya, sitaki fadhila yao !



Naomba nihurumiwe, yangu nikijifanyia,

Riziki nijipatie, ya halali ilokuwa,

Kivulini nijile, hata ni kavu ikiwa,

Mola wanaojifanya, sitaki fadhila yao !



Bure usijisumbue, vinono kuniletea,

Nenda navyo katumie, wewe kukusaidia,

Kiporo changu nachie, kukila naendelea,

Mola wanaojifanya, sitaki fadhila yao !



Mola wangu sio wewe, wala hauwezi kuwa,

Hili bora uelewe, vingine kutodhania,

Na moyo uufunguwe, ujue unaugua,

Mola wanaojifanya, sitaki fadhila yao !





No comments: