Sunday, November 18, 2012

Leo mnaowaabudu


KAENI mkitambua, ukweli utabakia,

Nasi tuliwaambia, hamkutaka sikia,

Miungu mnaozaa, watakuja waumbua,

Leo mnaowaabudu, watakuja kuwakana !



Sauti naisikia, ya saba inatokea,

Kukana mlilozua, kuwa yeye amezaa,

Uchuro aukataa, na wala hakuzaliwa,

Leo mnaowaabudu, watakuja kuwakana !



Warumi wawahadaa, yak wao kuyafatia,

Miungu wengi tabia, ndio wao walozua,

Wapenda kuwashindilia, kikapuni wakakaa,

Leo mnaowaabudu, watakuja kuwakana !



Kunaye wao wa mvua. na kisha kuna wa jua,

Huba naye kajaliwa, ana wake kawekewa,

Na wa mavuno hupewa, sadaka akaachiwa,

Leo mnaowaabudu, watakuja kuwakana !



Mola asikitikia, wasomi wasiosomea,

Hata kitu kukijua, na yakini kuitia,

Kama wana mnakuwa, uzushi ukawafaa ?

Leo mnaowaabudu, watakuja kuwakana !



Mola awahurumia, vitabu msiojua,

Moja mkajishikia, hakika lisilokuwa,

Kama vipofu kupewa, nafasi tembo kumjua,

Leo mnaowaabudu, watakuja kuwakana !



Yupo aliyeringia, tembo ni kama sinia,

Na mwingine kaingia, ujuzi ajivunia,

Kama shina anakuwa, tembo ninayemjua,

Leo mnaowaabudu, watakuja kuwakana !



Wote walijipatia, sehmu waliyoachiwa,

Zaidi hawakujua, kwingine kuyagundua,

Na Alamu muelewa, ndivyo anatufanzia,

Leo mnaowaabudu, watakuja kuwakana !









No comments: