Sunday, November 18, 2012

Taifa bovu



Watu wakinunuliwa, kuviwakilisha vyama,

Huwa mkubwa ukiwa, wa kukubali utumwa,

Kwani anayenunua, naye amenunuliwa,

Uwakilishi mbovu, huzaa taifa bovu!



IKiwatawala njaa, hamtojali uzima,

Chochote mtachukua, tumbo lipate heshima,

Ila utu hujivua, ukabakia mnyama,

Uwakilishi mbovu, huzaa taifa bovu!



Yote tumeyasikia, na wengine kutazama,

Watu wanawazomea, ukweli wanaosema,

Huko tunakoeleka, kuna ufu si uzima,

Uwakilishi mbovu, huzaa taifa bovu!



Taifa limeshapotea, hakuna wa kulitazama,

Wakubwa waliokuwa, nao kimya wanyamaa,

Nami ninajiulizia, kama wana nia njema ?

Uwakilishi mbovu, huzaa taifa bovu!



Vijana nawahofia, meli yao kwenda zama,

Hawa walionunuliwa, watawaacha salama,

Au nyie mwamjua, ni nini yake azma ?

Uwakilishi mbovu, huzaa taifa bovu!



Uwakilishi wa njaa, kazi yake ni kuzoma,

Akili unaishiwa, ukabaki kuzizima,

Twendako hawajajua, ni lipi tutalokwama,

Uwakilishi mbovu, huzaa taifa bovu!



Siasa wanadhania, ni sherehe kurindima,

Mapambo ya kuzingua, na rangi za kuparama,

Bila watu kuwalea, nchi hii itazama,

Uwakilishi mbovu, huzaa taifa bovu!



Wengine wanunuliwa, ya pombe kuyaegema,

Kauli za kupakua, ila kupika hukwama,

Nyuso wakazinyanyua, zisizofaa tazamwa,

Uwakilishi mbovu, huzaa taifa bovu!



Tambara hujiachia, halifai kulifuma,

Kelel zikizagaa, wapi uone hekima,

Vigezo visipotakiwa, wengine sio wazima,

Uwakilishi mbovu, huzaa taifa bovu!



Shangwe zikiendelea, taifa huwa kilema,

Mkongojo kuutwaa, ya heri kurudi nyuma,

Mbele ninayohofia, iliyojaa tuhuma,

Uwakilishi mbovu, huzaa taifa bovu!



Baraka zitapotea, na kukongoka rehema,

Watu wakadhulumiwa, ikapotea huruma,

Haki tukachuuziwa, na siasa za kichama,

Uwakilishi mbovu, huzaa taifa bovu!



Nyumba tunaibomoa, tena haina salama,

Macho ninayafumbua, kuzingojea zahama,

Nahofu kushtukia, nikakiona kiyama,

Uwakilishi mbovu, huzaa taifa bovu!





No comments: