Wednesday, November 14, 2012

WAJINGA WAKIAMKA

Walolala wakiamka, usingizi wakatoa,

Bongo zitahamanika, ukungu kuundoa,

Na yasiyoeleweka, yakaanza kuhojiwa,

Wajinga wakiamka, watamjua muongo !



Miaka wataitaka, hadithi kuhadithiwa,

Wengine walikofika, wapi walikoanzia,

Na nyie kilichoshindika, sababu mkaitoa,

Wajinga wakiamka, watamjua mjanja !



Malaysia wasifika, hata nasi twakujua,

Watoto twawapeleka, kwenda huko kusomea,

Mngefanza ya hakika, na sisi tungelikuwa

Wajinga wakiamka, watamjua mmbeya !



Indonesia wawika, vitenge tunanunua,

Na mashati kujivika, bichi tunapotumbua,

Haya hayakueleweka, wala hamkuyapania ?

Wajinga wakiamka, watamjua mnafiki!



Korea wamegawika, wa kwanza tunamjua,

Tulienda na dhihaka, njaa sasa wanalia,

Tukaachia hakika, leo walioendelea,

Wajinga wakiamka, watamjua mkweli !



Uchina tulikotoka, tofauti haikuwa,

Leo wanatuzunguka, mkiani twabamia,

Halafu wanawehuka, ustawi waujua ?

Wajinga wakiamka, watamjua muongo !



Yawapi ya Tanganyika, siku ilipoanzia,

Wakati tulipowika, dunia kutusikia,

Vipanya twatambulika, nani wa kutusikia ?

Wajinga wakiamka, watamjua mjanja !



Maji yanaadimika, hata kuliko maziwa,

Wakaishi kwa mashaka, maji kuyaaangalia,

Hata bomba kuchipuka, kazi kubwa imekuwa?

Wajinga wakiamka, watamjua mmbeya !



Pampu zimeshindika, wenyewe kujiundia,

Maji chini yalofika, nani aweza kutoa ?

Kisha unadanganyika, eti umeendelea ?

Wajinga wakiamka, watamjua mnafiki!



Umeme twaadhirika, kuzima na kuzimua,

Asilimia ya shaka, ndiyo tuliyojipatia,

Kwingine walazimika, gizani kuangalia ?

Wajinga wakiamka, watamjua mkweli !



Vijiji vimeuzika, kuzaa na kufulia,

Yao kwao tumepoka, giza tukawaachia,

Na dharau twaiweka, nani kuvitembelea ?

Wajinga wakiamka, watamjua muongo !



Barabara zaanguka, madaraja kutitia,

Reli zimeshakatika, vipande twajiungia,

Huko China wanawaka, umeme wanatumia ?

Wajinga wakiamka, watamjua mjanja !



Nani huyo alimaka. twaweza kuendelea,

Pasinapo kuuweka, umeme ukatumiwa,

Vijijini kujengeka, na miji ipate kua?

Wajinga wakiamka, watamjua mmbeya !



Mshamba yatalimika, kisegerrema kutumia ?

Majembe mliyonyaka, takataka yamekua,

Kilimo kwanza cha shaka, mbali hakitafikia,

Wajinga wakiamka, watamjua mnafiki!



Cha mwisho kitasifika, tusipoyaangalia,

Maana yaaminika, sipo tulipoanzia,

Kama kweli tengetaka, kuzalisha twatakiwa,

Wajinga wakiamka, watamjua mkweli !



Kama kweli tungetaka, kuzalisha twatakiwa,

Zana zenye uhakika, zikatoka Tanzania,

Mitambo ikajengeka, vifaa kufyatulia,

Wajinga wakiamka, watamjua muongo !



Vya msingi tukiweka, wenyewe twajiundia,

Itakuwa ni hakika. papo hapo twatokea,

Ila tukidanganyika hutajirisha dunia,

Wajinga wakiamka, watamjua mjanja !



Nyumba tunadanyanyika, watu kutowajengea,

Kazi hii ya hakika, haraka inatakiwa,

Kazi ikishamalizika, kujenga nchi inakuwa,

Wajinga wakiamka, watamjua mmbeya !



Madini twahadaika, wengine kuwaachia,

Sheria hatujaweka, wenyewe kujichimbia,

China yangelifanyika, wasingeliendelea,

Wajinga wakiamka, watamjua mnafiki!



Wajinga wakiamka, watataka kuelewa,

Mbona hamkushaurika, watu kwanza kuinua,

Kisha ndio mkazuka, ya kwenu kujifanzia,

Wajinga wakiamka, watamjua mkweli !



Mafisadi watataka, wote wakahesabiwa,

Na huko walikoyaweka, Uswizi tukakujua,

Porojo hawatataka, kwani waliishamua,

Wajinga wakiamka, watamjua mkweli !



Ninakumba Rabaka, kuyaondoa mashaka,

Siki ya watu kunyanyuka, rehema kutozizuia,

Kote zikamiminika, ubaya wema ukawa,

Wajinga wakiamka, watamjua mkweli !



Wote tukasalimika, kwa haki kuzingatia,

Yako yakakamilika, kati yaliyozuia,

Na wote walioponzeka, ya kwao waje fidiwa,

Wajinga wakiamka, watamjua mkweli !

No comments: