Sunday, November 18, 2012

Mshairi sikuhizi

Waliozoea hadhi, kwa ubwabwa na mandazi,

Washairi sikuhizi, huwa haviwapendezi,

Waelimika wajuzi, kuyatafuta azizi,

Mshairi sikuhizi, kaziye si kusifia,

Wanasonya viongozi, sasa wamnyanyapaaa !

Wanaotafuta mapenzi, wale sifa za Muizzi,

Kitu hawaokotezi, wakataa ubazazi,

Hali mashehe wa enzi, wafulia kwa hirizi,

Mshairi sikuhizi, kaziye si kusifia,

Wanasonya viongozi, sasa wamnyanyapaaa !

Ajijua si mkazi, majoho hayadarizi,

Wala siye muamuzi, ya watu hayatatizi,

Ajijua kiongozi, njia bora msimamizi,

Mshairi sikuhizi, kaziye si kusifia,

Wanasonya viongozi, sasa wamnyanyapaaa !

Huyu ni muangalizi, kuukataa ushenzi,

Tukamhofu Mwenyezi, na dunia kutoenzi,

Wala hanayo ajizi, yakitua mageuzi,

Mshairi sikuhizi, kaziye si kusifia,

Wanasonya viongozi, sasa wamnyanyapaaa !

Hakika ni muenezi, ya ovyo hayatangazi,

Asiyekwaza uwazi, iwe jana au juzi,

Ya umma ni mdowezi, haumalizi utenzi,

Mshairi sikuhizi, kaziye si kusifia,

Wanasonya viongozi, sasa wamnyanyapaaa !

Mipango ni msimamizi, mizuri si ya kichizi,

Kuyaleta mapinduzi, vya msingi kuvienezi,

Maji yakawa utenzi,usioisha simulizi,

Mshairi sikuhizi, kaziye si kusifia,

Wanasonya viongozi, sasa wamnyanyapaaa !

Chakula kikawa dozi, hakikosi mwanagenzi,

Vijiji wakapalizi, na mjini kuhifadhi,

Pakafanzwa na makuzi, uuzaji na uzuzi,

Mshairi sikuhizi, kaziye si kusifia,

Wanasonya viongozi, sasa wamnyanyapaaa !

Nyumba zataka ujenzi, kama la kwanza zoezi,

Watu ukiwahifadhi, mengine watafaridhi,

Pakiwa nayo ajizi, ufukara uko wazi,

Mshairi sikuhizi, kaziye si kusifia,

Wanasonya viongozi, sasa wamnyanyapaaa !

Hapanao utetezi, ila siasa chukizi,

Zitakazo kujienzi, na wengine kuwaizi,

Kwangu mimi machukizi, walal hazina hifadhi,

Mshairi sikuhizi, kaziye si kusifia,

Wanasonya viongozi, sasa wamnyanyapaaa !

No comments: