Wednesday, November 14, 2012

Kuringa kukigeuka


Mringaji 'kiringiwa, vipi anajisikia,

Mkausha kukaushiwa, macho vipi yanakuwa,

Na mnuna akununiwa, roho huwa yamtua ?

Kuringa kukigeuka, ikawa ni kuringiwa !



Haya ninaelezewa, bado ya kujionea,

Kama picha imekua, hisia zasisimua,

Ila yakinitokea, ukweli nitaujua,

Kuringa kukigeuka, ikawa ni kuringiwa !



Ukisha kuzuzuliwa, hukubali kuringiwa,

Kukiisha kuringiwa, hubakia na mafua,

Maana kilichokuwa, udhia kikabakia,

Kuringa kukigeuka, ikawa ni kuringiwa !



Mapamba yakikuhadaa, kehso yake hujijua,

Sio kitu ulokuwa, bado una yako njaa,

Jana uliyekimjua, leo hatokutambua,

Kuringa kukigeuka, ikawa ni kuringiwa !



Ndivyo ilivyo dunia, kuringa na kuringiwa,

Kila anayetumiwa, hataukwepa udhia,

Mifuko ikikujaa, mzuri huchukuliwa,

Kuringa kukigeuka, ikawa ni kuringiwa !



Mzuri huchukuliwa, mifuko inapokujaa,

Ila unaposhiwa, ubaya hutafutiwa,

Na mwisho ukazuliwa, hata chako kutwaliwa,

Kuringa kukigeuka, ikawa ni kuringiwa !



Dunia nguli wajaa, kazi yao ni ubaya,

Wanyonge huwaonea, na wale wasiojaliwa,

Thamani wakatolewa, na hasidi kupakiwa,

Kuringa kukigeuka, ikawa ni kuringiwa !

No comments: