Sunday, November 18, 2012

JAMBAWAZI WA UKWELI


Huyo huwa ni kibaka, jambawazi hatokuwa,

Mchana anayecharuka, jirani kuwaibia,

Uteja unampika, hamu budi kuridhia,

Jambawazi wa ukweli, haibii masikini !



Haibii masikini, jambawazi wa ukweli,

Huona ni uhaini, mkubwa uso mithali,

Wenzie hawamwamini, budi kumshtakia,

Jambawazi wa ukweli, haibii masikini !



Awajua masikini, vipi atawaibia,

Awanyime afueni, mautini kuwatia,

Kafiri na muumini, huiona ni hatia,

Jambawazi wa ukweli, haibii masikini !



Ukiwaona mjini, fukara wawaibia,

Uwajue kwa yakini, ni mateja walokuwa,

Kamwe hawana thamani, masikini kuibia,

Jambawazi wa ukweli, haibii masikini !



Wakatia mafichoni, Uswizi kwenda chimbia,

Huku njaa taabuni, kila mtu analia,

Ya kwao madhumuni, hakika ni kutuua,

Jambawazi wa ukweli, haibii masikini !



Wanatuona ni nyani, thamani wanatutoa,

Na vyao waamini, ndivyo vilivyojaliwa,

Hakika ni hayawani, wenda uchi pasi 'jua?

Jambawazi wa ukweli, haibii masikini !



Wa ukweli ajijua, kwa watu ataka nini,

Si kununua udhia, au wengine kuwahini,

Maisha ayaelewa, na uhai athamini,

Jambawazi wa ukweli, haibii masikini !





No comments: