Sunday, November 18, 2012

Tusingoje ya U.S.S.R.


U.S.S.R. jua, ilishaaga dunia,

Jambo hili latwambia, kitu tusichotambua,

Vigumu kufikiria, na gumu kuaminia,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Ni vipande imekua, hadithi twazisikia,

Waloleta ujamaa, walipojipendelea,

Ukweli ulipotua, wakaonwa ni wabaya,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Sasa stani zajaa,na kina Bylorussia,

Wapo kina Georgia, watu kunakozingua,

Pia nayo Chechnyia, watu wanayohofia,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Palikuwa na Rhodesia, hivi leo twasikia,

Zimbabwe na Zambia, ndizo hizo zilikuwa,

Kumbe nchi hujifia, kiyamache kikingia ?

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Ndivyo ilivyo dunia, yake inavyomboa,

Na asiyejitambua, hutaka kung'ang'ania,

Shauri asiposikia, haachi kujiumbua,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !

Si mbaya ujamaa, bali watu wa dunia,

Ujanja wakiutmia, matope hukupakaa,

Kizuri kilichokuwa, kuonekana kibaya,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Nchi zinakufa pia, ukitawala udhia,

Ngapi umezisikia, zimeiacha dunia,

Kumbuka Babylonia, zama ikihadithiwa,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Kunayo Mesopotamia, ilitawala dunia,

Uyunani nayo pia, wote tulishaelezewa,

Makuu waliyazua, mashine pasi gundua,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Misri twahadithia, ya zama ilivyokuwa,

Leo taka imekua, watu waona kinyaa,

Farao hajatokea, nchi kuja inyanyua,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Palikuwa na Persia, michezo twaisikia,

Mabinti waliong'aa, hadi wakapiganiwa,

Watu roho wakatoa, ili kwenda zawadiwa,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Palikuwa na himaya, Afrika twazijua,

Wachamungu kuwazua, kama Mali nasikia,

Hivi leo nayojua, si kitu ila balaa,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Marikani kulikuwa, na kubwa pia himaya,

Wahindi wakupakawa, huko walizinyanyua,

Dhahabu wakatumia, nyumba zao kujengea,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Tanganyika tuliua, mochwari hatukutoa,

Nimekwenda angalia, naona inapumua,

Na sauti kusikia, 'nawe utanipigania? '

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Naam, nikaitikia, bila ya kujitambua,

Labda nilihofia, maiti kuangalia,

Au baridi kukoa, kitu sikukitambua,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Kungi wanihadithia, mapenzi yanavyokuwa,

Mwana ukishamridhia, kambaye ni kumuachia,

Hunenda akatembea, au mbali kwenda kaa,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Ila kwawe kumuachia, huru atajisikia,

Ngamani atarejea, hema akalichimbia,

Na penzi juu likawa, hatolishusha radhia,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Kama ukimshikilia, na wivu tele kujaa,

Huyo atakukimbia, na wala hatarejea,

Ndivyo ilivyo dunia, mamboye ni kuyaachia,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Hili nilipogundua, mwepesi wa kuatia,

Usumaku nakataa, sitaki kung'ang'aniwa,

Biriani napindua, na kisha kuuachia,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Rangize kujitanua, chembe mojamoja kuwa,

Siniani kitulia, siriye hutoijua,

Sikio ukifungua, hunong'onezwa na jua,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



Mrima na Zanzibar, nadhani mwanisikia,

Uziwi sijaujua, hiyo nyingine balaa,

Naomba kutojaliwa, ili sote kujaliwa,

Hata nchi hufa pia, ukitawala udhia !



No comments: