Friday, November 2, 2012

Shemeji wenye hasidi

Ndoa zao huwa viza, na kitu wasifaidi,

Shemeji wanaoiza, za wengine kuhasidi,

Hata wanaojifanza, ni wa kweli maabudi,

Shemeji wenye hasidi, ndoa zao huwa viza!

Uwapende kama udi, na ubani kufukiza,

Roho imejaa tadi, yako hawachi kukwaza,

Wakaidhania sudi, kwao watatengeneza,

Shemeji wenye hasidi, ndoa zao huwa viza!

Nduguwe watawaponza, wawageuze gaidi,

Huhodhi nguvu za giza, kuwapandisha mdadi,

Kisha wakawachuuza, dini yao kuritadi,

Shemeji wenye hasidi, ndoa zao huwa viza!

Hao sio maliwaza, bali ni ya moto radi,

Ni adui sio wenza, ndoa wanaifasidi,

Na ni mkubwa muweza, yote kwao ni nakidi,

Shemeji wenye hasidi, ndoa zao huwa viza!

Hawamwogopi abadi, japo ibada wafanza,

Nyoyoni wameshadidi, ubaya kwako kufanza,

Na siku huja abadi, wenyewe kujilemaza,

Shemeji wenye hasidi, ndoa zao huwa viza!

Roho mbaya yao jadi, ndilo wanaloliweza,

Uhuni na ukuwadi, nyumba yao hutengeza,

Hakika hawafaidi, hata Idi huwazoza,

Shemeji wenye hasidi, ndoa zao huwa viza!

Wenyewe hujimaliza, wakadhani wafaidi,

Wivu huwa wawaponza, unaozaa hasadi,

Na kila wanalofanza, liwe halitaradadi,

Shemeji wenye hasidi, ndoa zao huwa viza!

Hili sio muujiza, falaqi inaahidi,

Akili anayetunza, na imani kuhimidi,

Humuogopa Muweza, wakaihofu hasadi,

Shemeji wenye hasidi, ndoa zao huwa viza!

No comments: