MBALI sana haijawa, toka karne kuishia,
Utumwani tulikuwa, watu tukinunuliwa,
Leo tena yarudia, yaleyale yalokuwa,
Watumwa wangelikuwa, elfu moja mia nane :
wajiuzao raia !
Kila unaloamua
Watu wanawatumia, fedha kuwamiminia,
Kisha wakazitumia, raia kuwanunua,
Ili kunyanyuliwa, huyo anayewanunua,
Watumwa wangelikuwa, elfu moja mia nane :
wajiuzao raia !
Yeye amejichagua, kati wote Tanzania,
Kuwa mafuta katiwa, na shetani tusomjua,
Mkubwa wetu kujakuwa, kuongoza Tanzania,
Watumwa wangelikuwa, elfu moja mia nane :
wajiuzao raia !
Ngawira ukigawiwa, usiache kupokea,
Mkono utautia, kinywani kuambulia,
Ila imani hofia, motoni kutoingia,
Watumwa wangelikuwa, elfu moja mia nane :
wajiuzao raia !
Ila imani hofia, motoni kutoingia,
Haramu kilichokuwa, huja kikawa mkaa,
Milele ukaungua, kwa visenti vya hadaa,
Watumwa wangelikuwa, elfu moja mia nane :
wajiuzao raia !
Kisha tena fikiria, kizazi kununuliwa,
Utaileta balaa, rushwa kote kusambaa,
Tukawa ni Nigeria, kwa masahibu na balaa,
Watumwa wangelikuwa, elfu moja mia nane :
wajiuzao raia !
Akili umejaliwa, watakiwa kutumia,
Kila anayenunua, naye amenunuliwa,
Hivi ni yake bidhaa, mwenzangu unaijua?
Watumwa wangelikuwa, elfu moja mia nane :
wajiuzao raia !
Thursday, November 8, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment