Sunday, November 18, 2012

Yangu hayana maana

Mimi daima mtwana, wala sijawa ni bwana,

Huo nilishaukana, kuritadi sina dhana,

Hunena ya kufanana, viumbe yakalingana,

Yangu hayana maana, ya kwao ndio yafaa !

Huwaachia mabwana, propaganda kuchuna,

Roho zao za ujana, bado zajaa hiana,

Wamkana maulana, utukufu kuuvuna,

Yangu hayana maana, ya kwao ndio yafaa !

Kwa yao ninapingana, uongo unaposana,

Kweli wakaitafuna, si ya leo siyo ya jana,

Ikawa yalia jana, kabla kila adhana,

Yangu hayana maana, ya kwao ndio yafaa !

Ikawalani amana, na kuiteza dhamana,

Yawarudi na wana, pasiwe na uungwana,

Mengine kutabanana, kwa usiku na mchana,

Yangu hayana maana, ya kwao ndio yafaa !

No comments: