Friday, November 2, 2012

Pepo za mabadiliko ...




SITINI zilipepea, uhuru kujipatia,

Bendera zikapepewa, uenyeji kuutia,

Weusi wakakitwaa, weupe walichotwibia,

Pepo za mabadiliko, nani atazizuia ?



Zimevuma na kulewa, na hewa zinagombea,

Mashimo yafyatuliwa, hewani yakabakia,

Vyombo sasa vyaelea,kuso dira kwelekea,

Pepo za mabadiliko, nani atazizuia ?



Tafakuri zajifia, ubaya waning'inia,

Wakubwa wanapepewa, siye j oto twaungua,

Zuri wakalikataa, na gizani kwelekea,

Pepo za mabadiliko, nani atazizuia ?



Kaskazini zaanzia, chini zinaelekea,

Kama kuta naambiwa, mkono ukitumia,

Kama ngumi waitia, viganja utaumia,

Pepo za mabadiliko, nani atazizuia ?



Kusini zinatokea, zinazodai usawa,

Katikati tumekaa, zinakuja kuingia,

Na wala hatujaamua, nini cha kujifanzia,

Pepo za mabadiliko, nani atazizuia ?



Pepo hizi zanua, kuiva demokrasia,

Kisha haki kutumia, si umbeya kusikia,

Vinginevyo ikiwa, wenyewe tutaumia,

Pepo za mabadiliko, nani atazizuia ?



Pepo zataka ruia, njia ya kuelekea,

Sio gizani twakaa, wengine wakijilia,

Harufu twaisikia, mlo hatujajionea,

Pepo za mabadiliko, nani atazizuia ?



Pepo hizi za kugawa, rasilimali kwa sawa,

Isiwe kuna waliwa, chakula wakingojea,

Kumbe juu wamekaa, wao wanaojilia,

Pepo za mabadiliko, nani atazizuia ?



Pepo zataka afua, na nafuu kuijua,

Na wala sio mafua, kikohozi kukohoa,

Na kuibadili tabia, ndyo dawa ya kufaa,

Pepo za mabadiliko, nani atazizuia ?



Pepo zataka usia, wa juu wakausikia,

Wakaiacha nazaa, na ubaya kuuzua,

Kwa vipi aso silaha, ni muanzisha ghasia,

Pepo za mabadiliko, nani atazizuia ?



Huyo ni wa kutania, mchezo wa mwana kulea,

Mkono ukimtoa, nani kukuangalia,

Kula asojitambua, hili hawezi kwelewa,

Pepo za mabadiliko, nani atazizuia ?



Pepo zimeshanuia, zama mpya kwingia,

Zaja kwa kufunguliwa, au zenyewe kufungua,

Hakuna wa kuzizuia, hili sana nalijua,

Pepo za mabadiliko, nani atazizuia ?



Nanyi mtajionea, yangu msiosikia,

Zaja zikisadiwa, kwa tufani na mvua,

Nchi tope itakuwa, mitaro tusipochimbua,

Pepo za mabadiliko, nani atazizuia ?



Minyororo tukitia, itakuja kuachia,

Kuna nguvu za dunia, zaendeshwa na ukiwa,

Katikati kiinngia, kinyamkera chaua,

Pepo za mabadiliko, nani atazizuia ?



Naihofia balaa, ninamuomba Jalia,

Yajayo kujitambua, njia bora kuchagua,

Tusijitie unaa, yakaja kutukong'oa,

Pepo za mabadiliko, nani atazizuia ?

No comments: