Thursday, November 8, 2012

Muogopeni Muumba





Muumba muogopeni, msiogope binadamu,

Amewaumba Manani, kwa ibada kumkimu,

Mengi hapa duniani, kwa haki yamdhulumu,

Muogopeni Muumba, msihofu binadamu !



Ya haki yaamueni, apate kuwarehemu,

Mkijifanya afkani, wenyewe mwajidhulumu,

Mtakuwa mashakani, akhera na duniani,

Muogopeni Muumba, msihofu binadamu !



Wanapozuka wahuni, nafsi kuwadhulumu,

Wao mkawathamini, na kuwaona muhimu,

Linamuudhi Bathini, na yake huwa adimu,

Muogopeni Muumba, msihofu binadamu !



Ni mkubwa mtihani, daima unaodumu,

Saburi na shukrani, akosaye hajihimu,

Ya kesho huwa haoni, aona ya uhadimu,

Muogopeni Muumba, msihofu binadamu !



Humpendeza shetani, na wala sio Karimu,

Akajitia thamani, kwa kuwa hajifahamu,

Kumbe yeye majinuni, na wala hajituhumu,

Muogopeni Muumba, msihofu binadamu !



Hujidanganya kundini, akajiona adhimu,

Kumbe si kitu duniani, hawezi kutakadamu,

Asubuhi na jioni, huwa inaisha zamu,

Muogopeni Muumba, msihofu binadamu !



Watakuja akhirini, nao piTa binadamu,

Wakaingia njiani, jukwani kuhudumu,

Kama wale wa zamani, na wote hatutadumu,

Muogopeni Muumba, msihofu binadamu !



Twendako tuogopeni, tulipo twapafahamu,

Huko kwetu ugenini, nani wa kutukirimu,

Miaka ihesabuni, si viumbe wa kudumu,

Muogopeni Muumba, msihofu binadamu !



No comments: