Sunday, November 18, 2012

Tutu, Kofi, Carter na Mary

Wazee mmechaguliwa, dunia kutumikia,

Heri ninawatakia, ya kwenu kufanikiwa,

Mola atawasaidia, kwa wengine kuwafaa,

Tutu, Kofi, Carter na Mary, Mola daim'awe nanyi !

Mwastahii radhia, heshima mliyopewa,

Kwani hamjapungukiwa, na jukumu mmetwaa,

Bila hata kulilia, zaidi juu kikawa,

Tutu, Kofi, Carter na Mary, Mola daim'awe nanyi !

Kote mnakotembelea,, baraka nawaombea,

Mguu wenu kuwa dawa, kila mnapoingia,

Na maneno nuru kuwa, wata njia wakajua,

Tutu, Kofi, Carter na Mary, Mola daim'awe nanyi !

Uzee watuzidia, inazeeka dunia,

Hili mkalitambua, na kati kuingilia,

Wengi sana twafulia, pasina wa kutwangalia,

Tutu, Kofi, Carter na Mary, Mola daim'awe nanyi !

Nchini mwetu wakaa, vya kwao wakajilia,

Pensehni wanapewa, nini kujihangaikia,

Ndipo walipofikia, mbali hawajaangalia,

Tutu, Kofi, Carter na Mary, Mola daim'awe nanyi !

Wazee wenzao pia, washindwa kuangalia,

Ila wawaachia wajanja kuwatumia,

Vizee vigange njaa, yao bila kutatuliwa,

Tutu, Kofi, Carter na Mary, Mola daim'awe nanyi !

Makubwa mkiaangalia, na madogo kuyajua,

Wanyonge wategemea, nafuu kujionea,

Dunia kuwasikia, kwenu nyie kupitia,

Tutu, Kofi, Carter na Mary, Mola daim'awe nanyi !

Dhaifu kusaidia, na wanyonge kuinua,

Wapate jitegemea, bila kuwategemea,

Uhai kumalizia, pasina ya kuumia,

Tutu, Kofi, Carter na Mary, Mola daim'awe nanyi !

No comments: