Sunday, November 18, 2012
Chema utakitambua
Hauachi kukijua, wema kilichojaliwa,
Ishara utazijua, ukianza na tabia,
Huziangalia hatua, kila anapotembea,
Chema utakitambua, kwa imani na tabia !
Mkamilifu radhia, kwa hulka na tabia,
Na moyoni ana hawa, wanyonge kusaidia,
Kujikweza hukataa, chini hutaka bakia,
Chema utakitambua, kwa imani na tabia !
Si wa kujitangazia, wala wa kujisifia,
Utumwa kauridhia, watu kuwatumikia,
Suti atazikimbia, na kanzu kujivalia,
Chema utakitambua, kwa imani na tabia !
Hariri hatochagua, ila pamba hutumia,
Daladala kupakia, gari akalikimbia,
Watu huwaangalia, si mali kukimbilia,
Chema utakitambua, kwa imani na tabia !
Anaijua dunia, kioo cha kutambia,
Kuvunjika yake njia, na vingine haijawa,
Yenyewe yabakia, watu hawatabakia,
Chema utakitambua, kwa imani na tabia !
Huishi akitambua, maisha kutumikia,
Kama watumikiwa, utumwa unaingia,
Mwenyewe atayavaa, na kisha akajivua,
Chema utakitambua, kwa imani na tabia !
Daima hujichekea, pasina kumtambua,
Tabasamu lake poa, vigumu kujionea,
Na anachokichekea, mwenyewe anakijua,
Chema utakitambua, kwa imani na tabia !
Dunia aishangaa, upepo kukimbilia,
Akili wanaopewa, wanashindwa jitambua,
Huko huko kuishia, hadi mvi kupaua,
Chema utakitambua, kwa imani na tabia !
Utani ajionea, jinsi tulivyoumbiwa,
Hakuna cha kubakia, majivu tu yabakia,
Kisha hujiangalia, akacheka na kulia,
Chema utakitambua, kwa imani na tabia !
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment