Friday, November 2, 2012

KAZI YANGUU KUSHAURI


KATIBA kuheshimiwa, gharama haitakuwa,

Ila mkiichezea, mengine huja kuzua,

Haki zikawa vichaa, zataka kujiinua,

Kazi yangu ushauri, katiba kuheshimiwa!



Yapo yaliyoruhusiwa, vipi mnaipindua,

Haki inapotolewa, nyie mkaichukua,

Huonekana nazaa, isiwe yaheshimiwa,

Kazi yangu ushauri, katiba kutochezewa!



Uamuzi mkitoa, pande zote kusikia,

Yenu msipoangalia, wengine huwachezea,

Adili wakapindua, kichwa chini vikakaa,

Kazi yangu ushauri, pande zote kusikia !



Wengine kama wambeya, wenzao husingizia,

Hao mkiwasikia, hatua mkachukua,

Mkenge mnaingia, halijatokea jua,

Kazi yangu ushauri, mshtaki kuhojiwa !



Sheria kuzipindua, tunaupanda karaha,

Na adha kujivunia, mepesi yaliyokuwa,

Miaka yakachukua, ya leo kuliamua,

Kazi yangu ushauri, kutochezea sheria !



Kipimo ninachukua, themometa kutumia,

Jawabu sintofikiria, wenyewe mtajionea,

Na hicho kilichokuwa, si vingine itakuwa,

Kazi yangu ushauri, wenyewe watayanena !



Ikiwa mwawahadaa, na wajinga kudhania,

Kisha wakayagundua, na ukweli kuujua,

Siwezi kuingilia, hilo wataloamua,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kuzungumza!



Ikiwa mwawaonea, na yao kuyazuia,

Kwa malengo kuhofia, na kisha kusingizia,

Wanazivunja sheria, hadi ndani kuwatia,

Nautoa ushauri, wenyewe kutafakari !



Enendeni Nigeria, mje kutusimulia,

Binadamu mkichaa, haki asipotendewa,

Hukubali kujiua, umalizike udhia,

Kazi yangu ushauri, darasa lenu dunia !



Kayaoneni Syria, bure yanayotokea,

Kitu hamtatumia, ila macho kujionea,

Watu ukiwanunua, ni rahisi kujiua,

Kazi yangu ushauri, kama damu mwahofia !



Maguvu mkikithiri, na utenzi wenye shari,

Mkavaa ujibari, na kuwatia kabari,

Mlazimishe hiari, kwa kuikosa saburi,

Kazi yangu ushauri, wenyewe watayapanga !



Mkikosa ushauri, kwa akili ufakiri,

Dhahiri ikadhihiri, kisirani na jeuri,

Pasiwe na umahiri, wala kutafuta shwari,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kutafakari !



Ikiwa mwawazuia, ya haki kujipatia,

Wakauona udhia, na hatua kuchukua,

La kwao likatimia, haramu kuwaambia,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kuyadhibiti !



Ikiwa mwawaibia, vya kwao mkachukua,

Na kisha mkajitia, vya kwenu vimeshakuwa,

Hilo wakilitambua, mimi pembeni nakaa,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kujitakasa !



Mali wakizichukua, nanyi mwawasadia,

Mimi nitashuhudia, ulimi sintofungua,

Ya mola ninatambua, mwenyewe ajilindia,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kujichunguza !



Watakapotambua, imani mnazigawa,

Zingine kupendelea, na zingine kuonea,

Viti juu vitakuwa, na meza zikaelea,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kuyapembua !



Kunyonya mkiaamua, wageni kuwaachia,

Kwao nitasimulia, na hadhari kuitoa,

Wala sintowakemea, mnalofanza mwalijua,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kupambanua !



Vijijini wakijua, vyao vilikamuliwa,

Mjini mwajijengea, vijiji vikafulia,

Na wana kuvikimbia, kilio wataangua,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kuomba radhi !



Ushirika wakijua, hila mlizitumia,

Uwezo ukalemaa, na watu kuukimbia,

Kwa siasa kuchimbia, dawa zisizokuwa,

Kazi yangu ushauri, wenyewe watachunguza!



Ahadi wakizijua, za ukweli hazikuwa,

Mitaro wataitia, nyuso zilizofubaa,

Na mvi kujiotea, kizazi hakijakuwa,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kufaragua !



Ujanja mktumia, watu kupandikizia,

Vitini kwenda lalia, haki wasioijua,

Imani wanaochezea, kwa shetani kuwavaa,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kusahihisha !



Udhaifu mkijua, na kisha kuachilia,

Yao yawe yanavia, na yenu kuendelea,

Hukumu wakiitoa, mimi nitaangalia,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kupeleleza !



Sauti mkizuia, watu kutowafikia,

Vitambaa kuwatia, ya kwao kutosikiwa,

Hilo nikilitambua, hapa nitajiondoa,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kujichunguza !



Elimu chini wakiwa, kwa shule zao kuua,

Ndani nitajisomea, kuitafuta dunia,

Wala neno sintotoa, wahaka kuwaachia,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kutafakari !



Afya wakizitumbua, kama vile vitumbua,

Kuvila mkakataa, na pembeni kutupia,

Ya watu mkiingia, yakiwafika mtajua,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kufikiria !



Uzaini mkitia, na hila kuzitumia,

Hadaa nitaijua, wala sintawaambia,

Ibaki kujionea, kile kitachotokea,

Kazi yangu ushauri, wenyewe watayafanza!



Uongozi ukivia, ugumba mkautia,

Kisha mkauridhia, umma kutokuufaa,

Mimi nitawashangaa, kisa sitaki kujua,

Kazi yangu ushauri, wenyewe watajipima !



Mchele mkichukua, na kisha mkaugawa,

Sawa kama imekuwa, au kama sio sawa,

Kilo sintoichukua, wenyewe ntawaachia,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kutathmini !



Watu mkiwanunua, kisha mkalikataa,

Mmetoa hamkutoa, wala sitaki elewa,

Ni yenu yaliyokuwa, mwapanda labda dawa,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kuyahakiki !



Silaha mkinunua, wapigwa wakalemaa,

Kodi waliyoitoa, ikawa inawaua

Nitakataa kulia, kicheko nitakitoa,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kutafakari !



Uchama mkitumia, taifa kujizuia,

Fikra nitainua, kwingine kuangalia,

Na wajinga kuwajua, jinsi wanavyochanua,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kuyaafiki!



Udugu mkijitia, adawa kukumbatia,

Na ndugu kumkimbia, adui mkadhania,

Langu nitawasusia, siwezi kuwaambia,

Kazi yangu ushauri, wenyewe watachunguza!



Salama mkiachia, hatari kwenda nunua,

Nyuma nitajirudia, hewa safi kupumua,

Hata kama nakujua, udugu nitajivua,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kutathmini !



Kamari mkitumia, ya kwenu kuyaamua,

Wenye fedha kuchagua, ili waje kuwafaa,

Bazazi wa kutojua, ujanja wawazidia,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kuyaamua!



KIla anayenunua, na yeye kanunuliwa,

Bwana ungelimjua, kitanzi ungejitia?

Ila ndani uki'ngia, nje hautajitoa,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kuyakataa!



Mkizipinda sheria, kwa rushwa kuabudia,

Uoza utachiua, maradhi kuwapatia,

Ila nitawakimbia, udhu usijepotea,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kuyakubali !



Gizani mkiingia, kutabana mkakaa,

Machoni 'tatia taa, moyoni kuangalia,

Na ukweli nikijua, nafsi nitaiua,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kujishaswishi!



Siku mkijitambua, na ukweli kuujua,

Moyoni kujiangalia, na hapo mlipofikia,

Haya mtayaelewa, bila kutafsiriwa,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kujikosoa !



Upofu mkitumia, uziwi mkajitia,

Ya kwenu msipojua, hukaangwa kwa hadaa,

Imani mkiijua, ya kweli yatachipua,

Kazi yangu ushauri, wenyewe watayafanza!



Hasira mkitumia, mkizi mtaishia,

Dauni kutumbukia, msiweze kujitoa,

Akili mkitumia, ya kwanu mtaandaa,

Kazi yangu ushauri, wenyewe watatengeza !



Mikakati mtajua, ya nyakati kutumia,

Kwa safu kujipangia, kama mlivyoamriwa,

Amiri kutangulia, na nyie mkafatia,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kujiuliza !



Umoja pasipokuwa, ovyo mtachambuliwa,

Bongo msipotumia, miili mtaiua,

Yafaa kufikiria, kisha ifate hatua,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kurekebisha !



Laiti ningelijua, haiwi ni kabilia,

Daima ni baadiya, kwa kila mwenye kujua,

Na miaka yafikia, haya mtaja yajua,

Kazi yangu ushauri, wenyewe kutekeleza!





No comments: