Thursday, November 8, 2012
VICHOCHORO NAVIJUA
Bure mwapotea njia, kwa kushindwa ulizia,
Ububu mnajitia, kiburi uliokoa,
Kila mnachotumia, bure ninajipatia,
Njooni mwonyeshwe njia, vichochoro navijua !
Katika hii dunia, ya kula na kugawia,
Mwenyewe ukijilia, wengine walale njaa,
Mwisho watakumbia, mwenyewe ukabakia,
Njooni mwonyeshwe njia, vichochoro navijua !
Kila mwenye kujijua, kamba refu huachiwa,
Vyema apate potea, asifike kwelekea,
Kinyume kwenda ingia, mbali akapotelea,
Njooni mwonyeshwe njia, vichochoro navijua !
Wapo wanaozaliwa, vibaya wakalelewa,
Tabaka wakanunua, juu wawe waelea,
Hata ya kusalimia, kwayo wawe waugua,
Njooni mwonyeshwe njia, vichochoro navijua !
Ndipo yanapotukia, ya kushindwa ulizia,
Kujua wakajitia, njia wasiotambua,
Mkenge kwenda ingia, kama si mmamba kuwa,
Njooni mwonyeshwe njia, vichochoro navijua !
Ofa ninawagawia, wasiyoitegmeea,
Kubalini kutojua, wapo wa kuwasaidia,
Yote tukayachambua, na njia kuigundua,
Njooni mwonyeshwe njia, vichochoro navijua !
Miaka imesalia, michache iliyouwa,
Hadaa kwa teknolojia, hapo mwaja kufulia,
Ndimu zilizokomaa, chachu yake hupungua,
Njooni mwonyeshwe njia, vichochoro navijua !
Chachu yake hupungua, kama chungwa kuja kuwa,
Kama ukilikamua, juisi hujipatia,
Hili ninawaambia, mpate kufikiria,
Njooni mwonyeshwe njia, vichochoro navijua !
Fikra ukiishiwa, huwa ni ngumu dunia,
Usiwe wajitambua, kuwa uchi umekaa,
Uwe unajidhania, suti bora umevaa,
Njooni mwonyeshwe njia, vichochoro navijua !
Malezi mwana kulewa, ajizi nyumba ya ukiwa,
Halisimami gunia, tupu lililobakia,
Na hauwaki mshumaa, pasina kujiwashia,
Njooni mwonyeshwe njia, vichochoro navijua !
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment