Sunday, November 18, 2012

Tukaishi vijijini



Vijiji twavikimbia, sana mbali vimekaa,

Hakuna kwenda kukaa, sikuzote kutembea,

Kwalo ninalishangaa, vipi vitaendelea ?

Tukaishi vijijini, kuyaleta mapinduzi !



Kila mtu kaamua, mjini kukimbilia,

Serikali na jamaa, yao moja limekuwa,

Sasa watu waingia, na jioni kuambaa ?

Tukaishi vijijini, kuyaleta mapinduzi !



Kila nikiangalia, hduuma nazigundua,

Sana zimeshafulia, na kisha kuchafuliwa,

Hali yadharauoiwa, kukaa wanakataa,

Tukaishi vijijini, kuyaleta mapinduzi !



Maji safi nahofia, kwingi yameshapotea,

Bomba zimeshachakaa, ardhini yakimbilia,

Palipo nalo jipya, kuti kavu wakalia,

Tukaishi vijijini, kuyaleta mapinduzi !



Umeme wahadithiwa, lini kuja kuingia,

Mahala ukitokea, watu washerekea,

Miaka ingelikuwa, tayari unatolewa ?

Tukaishi vijijini, kuyaleta mapinduzi !



Huduma za kutitia, kwa elimu na afya,

Kiwango chini watoa, mizania yakataa,

Kila ukifikira,kizazi kinaonewa,

Tukaishi vijijini, kuyaleta mapinduzi !



Sasa nimeshaamua, kijijini kwelekea,

Na karibu naitoa, kwa wanaofatilia,

Naenda kusaidia, viwango kuvinyanyua,

Tukaishi vijijini, kuyaleta mapinduzi !



Pwani naenda anzia, vijiji kuzungumzia,

Hoja nimejipangiwa, udhaifu naujua,

Kama wakinisikia, pamoja kuendelea,

Tukaishi vijijini, kuyaleta mapinduzi !



Naitaka jumuiya, ya kwake kuangalia,

Akili kuzitanzua, tuanzapo kupajua,

Na kisha kuvichambua, vifaavyo kujifanzia,

Tukaishi vijijini, kuyaleta mapinduzi !



Maji la kwanza likawa, kijijini kuingia,

Kisha nyumba kuandaa, mkakati wa kuzua,

Kufumba na kufumbua, kijiji kipate ng'aa!

Tukaishi vijijini, kuyaleta mapinduzi !



Huduma zikafatia, ili kilimo kukua,

Usafiri kuutia, urahisi kuridhia,

Kisha tukaangalia, wengine kuwavutia,

Tukaishi vijijini, kuyaleta mapinduzi !



Utalii kutumia, kipato kuongezea,

Huku ninajisomea, na vitendo kuvizua,

Naikataa nadharia, feli nimeziamua,

Tukaishi vijijini, kuyaleta mapinduzi !



Mola ninamlilia, ndoto zangu kuridhia,

Kusoma huku kukawa, kunaleta manufaa,

Jamii ikichanua, na moyo wangu kuchanua,

Tukaishi vijijini, kuyaleta mapinduzi !







No comments: