Friday, November 2, 2012

Mbegu za demokrasi

Tisini nimeanzia, mbegu hizi kuzigawa,

Mwanzoni kwenye ukiwa, watu hawakuelewa,

Hivi sasa yamekua, na wenyewe wanunua,

Mbegu za demokrasi, nimegawa kapandeni !

Kumbukumbu maridhia, na mimi nilichangia,

Kidogo kilichokuwa, kama tukifanikiwa,

Kulea demokrasia, na dikteta kuzuia,

Mbegu za demokrasi, nimegawa kapandeni !

Vyama vingi kuanzia, hadi vilipoingia,

Mbegu nimezitia, kitabu cha Tanzania:

Chama kimoja mwaa, vyama vingi kuwa njwaa,

Mbegu za demokrasi, nimegawa kapandeni !

Katiba tukaingia, watu wabana kimya,

Hadi wakastuliwa, kelele nilipotoa,

Haraka yakaundiwa, yawe na yasiyokuwa,

Mbegu za demokrasi, nimegawa kapandeni !

Hapa kwenu kuchangia, mjitokeze Tanzania,

Mawazo bora kutoa, katibani kuingia,

Fursa kutoachia, la kwako kutojaliwa,

Mbegu za demokrasi, nimegawa kapandeni !

Tume nayo kufatia, katiba halijaishia,

Sababu sijaijua, kwnaini tunachelewa,

Haki inayolaliwa, ni dhuluma inayokua,

Mbegu za demokrasi, nimegawa kapandeni !

Kisha huru mgomeba, haraka kuamuliwa,

Uchumi kusaidia, mafedha wakayawa,

Waliojaa tamaa, hapa hawatachelewa,

Mbegu za demokrasi, nimegawa kapandeni !

Moyo huwasukumia, haraka wakaingia,

Na wakisha kununua, hamna kujivunia,

Ndivyo inavyotakiwa, kustawi demokrasia,

Mbegu za demokrasi, nimegawa kapandeni !

Kuwa chini ya sheria, rais pia raia,

Vingine haitofaa, mchezo tutachezewa,

Nani wa kuaminiwa, katika hii dunia,

Mbegu za demokrasi, nimegawa kapandeni !

Kipato kukiamua, nani zaidi kupewa,

Daktari kuchagua, au mwalimu kupewa,

Na wabunge kuamua, walipwe kwa tasnia,

Mbegu za demokrasi, nimegawa kapandeni !

Wanasiasa balaa, cha juu wakiambua,

Ovyo wanakitumia, hongo kote kuzitoa,

Mno twawazidishia, kufuru wajifanzia,

Mbegu za demokrasi, nimegawa kapandeni !

Katiba inatakiwa, sawa kutuwekea,

Watu wakaendelea, si kwa siasa kuingia,

Ila pale walipokuwa, juu waweze fikia,

Mbegu za demokrasi, nimegawa kapandeni !

Juu waweze fikia, siasa chini zikawa,

Wachache kukimbilia, kama Norway ilivyokuwa,

Huko ni wenye nia, ya watu tu kufaa,

Mbegu za demokrasi, nimegawa kapandeni !

Elimu nategemea, ya bure kujifanzia,

Madini ya Tanzania, na mafuta yaingia,

Fedha zake kutumiwa, wana kutusomeshea,

Mbegu za demokrasi, nimegawa kapandeni !

Afya na tiba pia, bure budi kutolewa,

Ni huduma ya jamaa, kila mtu hufikia,

Siku akahitajia, asiikose raia,

Mbegu za demokrasi, nimegawa kapandeni !

Rushwa mkiikataa, na usafi kulilia,

Mahala itafikia, nchi bora hii kuwa,

Namimi nawaombea, Mola kuwasaidia,

Mbegu za demokrasi, nimegawa kapandeni !

No comments: