Wednesday, November 14, 2012

Wote adawa wakiwa


Wote adawa wakiwa, rafiki awe ni nani ?

Hivi unafikiria, au sasa hayawani ?

Kuua na kuuliwa, iwe ndio yako shani ?

Wote adawa wakiwa, utachukia dunia !



Unaweza kupagawa, ukaingia kichaa,

Mafuu ukishakuwa, huna utalotambua,

Utaabiri mitaa, makopo kuyaepua,

Wote adawa wakiwa, utachukia dunia !



Shuruti yakutumia, kama maji ni kupoa,

Kuna njia hufikia, pemeni kujikalia,

Hali ukaichungua, wapi unaelekea,

Wote adawa wakiwa, utachukia dunia !



Ndipo unapogundua, binadamu ni hadaa,

Machoni kajifichia, na moyoni kuitia,

Akaifua na haya, na aibu kuitoa,

Wote adawa wakiwa, utachukia dunia !



Hutaka kukutumia, na wala si kumtumia,

Kila akikusadia, lake anafikiria,

Aweza akalichopoa, haraka kujiondoa,

Wote adawa wakiwa, utachukia dunia !



Mwema nawakubalia, watunzi waliyozua,

Hakika hajazaliwa, ila waovu wajaa,

Hii ni yetu dunia, ndio mambo yake haya,

Wote adawa wakiwa, utachukia dunia !



Waongo hukuzidia, ndiyo juu wakakaa,

Wewe ukawadhania, ndio wanaokufaa,

Kumbe wanakutumia, wende walikokukusudia,

Wote adawa wakiwa, utachukia dunia !



Yako ukenda fulia, hilo halitosumbua,

Ya kwanza kuangalia, ndio ahadi watiya,

Vingine haitakuwa, laiti ungelijua ?

Wote adawa wakiwa, utachukia dunia !









No comments: