Sunday, November 18, 2012

Mtumwa akishalewa


Mtumwa akishalewa, shairi hujitungia,

Pombe akaisifiwa, na mpishi kupambiwa,

Kisha akawarukia, uhuru wanaolilia,

Mtumwa akishalewa, uhuru ataucheka !



Kicheko hukiangua, habari akisikia,

Kuna wanaolilia, uhuru kujipatia,

Ya kwao wakaamua, wapate kuendelea,

Mtumwa akishalewa, uhuru ataucheka !



Senti imemlevyea, hawezi jielewa,

Kichwani imeingia, ya kutunzwa na kupewa,

Uimbaji anajua, bwanawe kumsifia,

Mtumwa akishalewa, uhuru ataucheka !



Hii ni yenu dunia, mbingu sijaandikia,

Huku yao wnajua, uhuru walishapewa,

Ila nyie wa kuwia, msiowia raia,

Mtumwa akishalewa, uhuru ataucheka !



Mtumwa anaridhia, bwanawe kumtumia,

Chakula akipatiwa, hanalo la kuamua,

Kutumwa anangojea, kwingine asokujua,

Mtumwa akishalewa, uhuru ataucheka !



Shurubu huidhania, yeye ameandikiwa,

Ndivyo alivyozaliwa, lingine kutotegemea,

Mnyenyekevu huwa, hata panapo udhia,

Mtumwa akishalewa, uhuru ataucheka !



Hujikunyata mkiwa, mama akitulkaniwa,

Uso akakumbatia, milizamu kuzuia,

Huwa anafikiria, haki yake inakuwa,

Mtumwa akishalewa, uhuru ataucheka !



Haki yake inakuwa, yeye akatukaniwa,

Kisha akadhulumiwa, na budi kuitikia,

Vingine akiamua, ni mkosa yeye huwa,

Mtumwa akishalewa, uhuru ataucheka !



Huituhumu dunia, kuwa inamuonea,

Kumbe yeye karidhia, kile kisichoridhiwa,

Na tokea kuzaliwa, ni huru aliyekuwa,

Mtumwa akishalewa, uhuru ataucheka !



Dunia ihofia, kuwa itamchezea,

Akashindwa kutambua, akili katunukiwa,

Naza akizitumia, ufukara huua,

Mtumwa akishalewa, uhuru ataucheka !



Wanaokung'ang'ania, kuna lao waambua,

Fika wanalitambua, hasara kukuachia,

Mwenye njaa wanjua, ni rahisi kutumiwa,

Mtumwa akishalewa, uhuru ataucheka !



Ndivyo ilivyo dunia, wajinga hufurahia,

Hawajengi huezua, hata waliyojengewa,

Wa kale wangelikuwa, haya wangeliyakataa,

Mtumwa akishalewa, uhuru ataucheka !



No comments: