KIU wengi wazidiwa, maji wanayalilia,
Na wanayoyasikia, miradi wakipangia,
Ila hat alile la dawa, maji hayajaingia,
Leo hii Tanzania, sio nchi ya furaha !
Waishi Watanzania, hata kando ya maziwa,
Nako ni kizaazaa, maji pia yapotea,
Wengine wayachukua, kwenda kwao kuwafaa,
Leo hii Tanzania, sio nchi ya furaha !
Maji wengi twafulia, sio kwa kusafishia,
Ila nayo kutokuwa, na uchafu unajaa,
Sasa dhiki imekua, hata ua kunyweshea,
Leo hii Tanzania, sio nchi ya furaha !
Chakula chazidi paa, bei twashindwa fikia,
Na hali ukiangalia, ukali waendelea,
Itakuja kufikia, mlo kutoambulia,
Leo hii Tanzania, sio nchi ya furaha !
Shangwe ninazihofia, zisijekuwa kulia,
Matumbo yakiadhiriwa, hifadhi kutopatiwa,
Vijijini wakavia, zaidi kudhulumiwa,
Leo hii Tanzania, sio nchi ya furaha !
Gizani tunaingia, asubuhi kuamkia,
Na nyimbo tunasikia, tatizo kuliondoa,
Miezi inaishia, hadithi yaendelea,
Leo hii Tanzania, sio nchi ya furaha !
Mashine wazilipua, katakata kwendelea,
Hakuna wa kufidia, mtenzi azawadiwa,
NI za kichizi sheria, laiti wangezijua,
Leo hii Tanzania, sio nchi ya furaha !
Kweli wapo wa kung'aa, njia zao wazijua,
Hawa ukijionea, pepo utaidhania,
Ila wengi ninajua, hali leo zawaua
Leo hii Tanzania, sio nchi ya furaha !
Siwezi jihurumia, afadhali naijua,
Nyuma sijaangalia, naitafuta afua,
Ninamsihi Jalia, hili kujaniridhia,
Leo hii Tanzania, sio nchi ya furaha !
Gharama zazidi paa, kwa elimu na afya,
Mikopo yatukimbia, wakubwa kuwafatia,
Kile tunachobakiwa, yabidi kupigania,
Leo hii Tanzania, sio nchi ya furaha !
Ni huzuni imekuwa, tena mkubwa ukiwa,
Kesho tunaihofia, jinsi itakavyokuwa,
Utabiri nakimbia, mimi siwezi kutoa,
Leo hii Tanzania, sio nchi ya furaha !
Mola ninamuachia, kadari kuiangalia,
Dhiki kutuepushia, toba zetu kisikia,
Nasi tuongeze dua, tupate kuhurumiwa,
Leo hii Tanzania, sio nchi ya furaha !
Wednesday, November 14, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment