Friday, November 2, 2012

Kwa moyo msifikiri




AKII ziajirini, muwe nayo itihari,

Mnayobeba moyoni, yafaa kutahadhari,

Mengine ya usononi, tena mkubwa hatari,

Kwa moyo msifikiri, akili ziajirini.



Sura ziangalieni, na utu muutabiri,

Kuna vichaa kundini, maisha watahasiri,

Hao macho wajueni, wanashinda makafiri,

Kwa moyo msifikiri, akili ziajirini.



Ya moyo hatuyaoni, ila mnachoabiri,

Na akili si usoni, inahifadhi suduri,

Vitendo angalieni, mengine huwa dhahiri,

Kwa moyo msifikiri, akili ziajirini.



Moyo una mtihani, ya rushwa na utajiri,

Kibaya ukathamini, kwa sura kuihasiri,

Kumbe waendo motoni, ukajiona ni kheri,

Kwa moyo msifikiri, akili ziajirini.



Yafaa kutathmini, na hofu kuidhikiri,

Msiingie utani, yakaja kuwaadhiri,

Angani na baharini, kote muondoe shari,

Kwa moyo msifikiri, akili ziajirini.



Maisha ni kubaini, na vyema kutafsiri,

Wala sio yaniyani, mapenzi yenye ghururi,

Nje yanakuwa shani, ndani hayana fahari,

Kwa moyo msifikiri, akili ziajirini.



Maisha ni mitihani, ya ubaya na uzuri,

Hushawishi uhaini, kwa thamani za sifuri,

Waishi waso anwani, wenye nazo kughairi,

Kwa moyo msifikiri, akili ziajirini.



Maisha ni ihasani, yafaa kutafakari,

Hili ukilibaini, waweza kutasawari,

Ukishaila yamini, uendako ni kuzuri,

Kwa moyo msifikiri, akili ziajirini.



Kanituku Manani, kipaji chenye urari,

Kweli nikaiamini, kwa fahari ya Kahari,

Na kulea madhumuni, yaso shari bali kheri,

Kwa moyo msifikiri, akili ziajirini.



No comments: