Wednesday, November 14, 2012

mwanzo wa kuheshimiwa

UCHAFU ukiingia, nyingine hakuna dawa,

Bali kuzawa upya, ya kwanza ukaanzia,

Na nani atakwambia, ya kwanza yanavyokuwa ?

Ni upya ukizaliwa, mwanzo wa kuheshimiwa !

Na nani atakwambia, ya kwanza yanavyokuwa ?

Kuanzapo yatakiwa, kishake yakachanua,

Na jinsi ya kuyalea, ujana ukarejea?

Ni upya ukizaliwa, mwanzo wa kuheshimiwa !

Huanza kwa kuchungua, walo safi kuwajua,

Kisha ukawaachia, safu wakajipangia,

Wenyewe wanajijua, wengine wasiojua,

Ni upya ukizaliwa, mwanzo wa kuheshimiwa !

Usafi waliojaliwa, nyuso zao zinang'aa,

Unafiki ukitoa, hutoacha kuwajua,

Nao wakikuanglia, macho utayakimbia,

Ni upya ukizaliwa, mwanzo wa kuheshimiwa !

Ni rahisi kuwajua, kama dhambi wakimbia,

Na shetani wamtoa, ashindwe na kulegea,

Hao wanapobakia, malaika huingia,

Ni upya ukizaliwa, mwanzo wa kuheshimiwa !

Mtume hawatojitia, au unabii kuzua,

Dhaifu wanaokuwa, tena kimya wakaa,

Watu wakaangalia, jinsi wakijipitia,

Ni upya ukizaliwa, mwanzo wa kuheshimiwa !

Wametosheka radhia, na Mola awafurahia,

Yao amesharidhia, na milango kfuungua,

Kiburi msipotia, hamuachi watambua,

Ni upya ukizaliwa, mwanzo wa kuheshimiwa !

No comments: