Sunday, November 18, 2012
DHAMANA
Ukubwa mkiupewa, wakubwa hamjakuwa,
Vibaya mwachukulia, hicho mnachoachiwa,
Madaraka huachiwa, sio ya kuyachukua,
Zirudisheni dhamana, sio yenu mamlaka !
Mwaachiwa kutumiwa, kwa haki inavyokuwa,
Nyenzo hii hutumiwa, walio wengi kufaa,
Ndipo sawa inakuwa, sio vingine kwamua,
Zirudisheni dhamana, sio yenu mamlaka !
Wewe ukiiutmia, mwenyewe kutumikiwa,
Ukapata manufaa, halali yasiyokuwa,
Ni wizi watumia, wala sawa haijawa,
Zirudisheni dhamana, sio yenu mamlaka !
Kaziyo kutumikia, na sio ya kutumiwa,
Kama hivyo inakuwa, unaianza balaa,
Vipi kukuchukulia, kiongozi ulokuwa ?
Zirudisheni dhamana, sio yenu mamlaka !
Yataka kujisimamia, la halali kulijua,
Muumba akakujua, uongozi wakufaa,
Sio ukanyenyekea, kile tusichokijua,
Zirudisheni dhamana, sio yenu mamlaka !
Mamlaka ya raia, haki inavyotambua,
Katiba inalijua, waziwazi linakuwa,
Ila huzuka hadaa, watu wakazainiwa,
Zirudisheni dhamana, sio yenu mamlaka !
Wenye vyeo kudhania, nchi yao imekuwa,
Ovyoovyo kuamua, na ya kweu kukataa,
Hilo mwisho lafikia, macho wameshayafungua,
Zirudisheni dhamana, sio yenu mamlaka !
Heri hili kutambua, tujenge demokrasia,
Ya kweli iliyokuwa, wala sio ya snaa,
Mida imeshaingia, mageuzi kuingia,
Zirudisheni dhamana, sio yenu mamlaka !
Pepo zinakurubia, nafasi kuichukua,
Ombwe nje kulizoa, la haki kuzingatiwa,
Mwaka hautoishia, mengi tutayasikia,
Zirudisheni dhamana, sio yenu mamlaka !
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment