Wednesday, November 14, 2012

H A T A U V A E H A R I R I


Pendeza namna gani, hilo halitakufaa,

Wakikutambua n yani, tabia zimelegea,

Hukuona hayawani, wote wakakukimbia,

Hata uvae hariri, mchafu ukishakuwa:

Watu watakukimbia !



Libasi huficha soni, aibu pia na haya,

Asiyekuwa yakini, thamani humpungua,

Huonekana ni duni, ngamiani kubakia,



Hulka kubwa thamani, kiumbe huongezewa,

Ukiikosa amini, kitu hauwezi kuwa,

Na hata ukiwa nani, kuanguka si hatua,

Hata uvae hariri, mchafu ukishakuwa:

Watu watakukimbia !



Maisha kama kanuni, hili huliangalia,

Halirdhii shakani, watu wanalolitia,

Huliachia fukweni, tengani hawatotia,

Hata uvae hariri, mchafu ukishakuwa:

Watu watakukimbia !



Hayo ndiyo madhumuni, kwa wote wasiojua,

Vingine ni uhaini, kila mtu anajua,

Waufanzao utani, kesho hawajaijua,

Hata uvae hariri, mchafu ukishakuwa:

Watu watakukimbia !



Ismaili wala suni, hili hawajakataa,

Wamefanyia yamini, ashura kuiandaa,

Usafi wautamani, kujiosha ndiyo njia,

Hata uvae hariri, mchafu ukishakuwa:

Watu watakukimbia !



Hujihini masikini, hata tambara kuvaa,

Isipokuwa moyoni, shaka wakaiondoa,

Usafi kujiamini, hata wakidharauliwa,

Hata uvae hariri, mchafu ukishakuwa:

Watu watakukimbia !



Hawanao usononi, ya dunia kuyavaa,

Wajua ya utumwani, hadimu kujisikia,

Akawa na majivuni, mabwana kutumikia,

Hata uvae hariri, mchafu ukishakuwa:

Watu watakukimbia !



Nakushukuru manani, kwa kaniki kuivaa,

Nguo hii ya peponi, hariri hugeukia,

Tutapokaa vitini, huku tunahudumiwa,

Hata uvae hariri, mchafu ukishakuwa:

Watu watakukimbia !





No comments: