Sunday, November 18, 2012

Sherehe zingine baa

Hali usipoangalia, mwenyewe ukajifaa,

Waweza kushangilia, ujikute wazomewa !

Na hasa palipo njaa, uhitaji na ukiwa,

Sherehe zingine baa, zinajenga kuchukiwa !

Hali ukiangalia. busara zinatakiwa,

Sahihi kuliamua, kwa wakati kutambua,

Mengine ukiyazua, lawama wajitakia,

Sherehe zingine baa, zinajenga kuchukiwa !

Hata uwezo ukiwa, watakiwa achilia,

Shida ukairidhia, kwa mithili kuitia,

Mnyonge kutougua, na laana kufyatua,

Sherehe zingine baa, zinajenga kuchukiwa !

Jirani hawezi fiwa, wewe ukashereheka,

Mchawi hukudhania, kama hilo hujajua,

Hekima ukijaliwa, mapema huligundua,

Sherehe zingine baa, zinajenga kuchukiwa !

No comments: