Thursday, November 8, 2012
MSAMBE SIKUTETA
Njia nimeipitia, na mwisho sikuishia,
Mimi ni mpita njia, wengine ninaachia,
Niliyokwishapangiwa, yaishia kutimia,
Msambe sikuyateta, mkajitia uziwi !
Akili nilifungua, ukweli kuangalia,
Niliikuta hadaa, kona zoe imejaa,
Nchi inauogea, na wengine wafulia,
Msambe sikuyateta, mkajitia uziwi !
Mengine nilidhania, kinyume chake ikawa,
Maji yalinikatalia, kwenye gunia kujaa,
Tope yameniachia, miguu kunichafua,
Msambe sikuyateta, mkajitia uziwi !
Na kila mnunuliwa, sasa ananichukia,
Kafara kuikataa, mizimu haikutwaa,
Hakuna kilichobakia, uoza umebakia,
Msambe sikuyateta, mkajitia uziwi !
Yapo yasiyojaliwa, kisirani yanakuwa,
Balaa kutangulia, zahama nayo mabaa,
Wafu huja kuzaliwa, na vichanga kufukiwa,
Msambe sikuyateta, mkajitia uziwi !
Nuru wenyewe huua, giza wakashangilia,
Linapowaelemea, wakashindwa vumilia,
Wakawa watu wa kulia, kushoto wasiojua,
Msambe sikuyateta, mkajitia uziwi !
Shetani msipomkimbia, yeye hatowakimbia,
Ukuraba ni furaha, apenda kufurahia,
Ila hukumu ikiwa, nyie atawakimbia,
Msambe sikuyateta, mkajitia uziwi !
Vipofu nashuhudia, haya walijionea,
Na viziwi kusikia, Tanzania italia,
Ila hawakuyasikia, wale waliotegemewa,
Msambe sikuyateta, mkajitia uziwi !
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment