Sunday, November 18, 2012

Binadamu sio hai



Watu wasiofikiri, kazi yao kuitika,

Kwa muda huwa mazuri, yao yanapofanyika,

Ili wakati hutua, mambo yakaharibika,

Binadamu sio hai, fikra zinapozikwa!



Ukiuua kufikiri, na wewe unajiua,

Huo sio umahiri, hakika ni kulemaa,

Hulikimbia la heri, shari ukaivamia,

Binadamu sio hai, fikra zinapozikwa!



Watu watayakariri, yale ya kushangilia,

Wasiwe na itihari, misingi kuitambua,

Hujichimbia kaburi, huku waangalia,

Binadamu sio hai, fikra zinapozikwa!



Baharini husafiri, bila kinga kuchukua,

Wao wakatafsiri, chama kilishaamua,

Na papa wawasubiri, mrama wakiingia,

Binadamu sio hai, fikra zinapozikwa!



No comments: