Thursday, November 8, 2012
Kukomoana
Mswahili anajua, kinyozi huwa hajinyoi,
Labda ingelikuwa, kwa mashine yuko hai,
Bali hilo ninajua, kwenda mbele hajawahi,
Usinikomoe mimi, ukajikomoa wewe !
Hapa tulipofikia, hili siwakubalii,
Kazi yangu kuchochea, kutafuta ustawi,
Vya watu mkitumia, kitu hamuambulii,
Usinikomoe mimi, ukajikomoa wewe !
Humshangaa mjua, aliyekuwa hajui,
Ujibari kujitia, sumu asiikinai,
Lusifa hajatambua, ni rafiki si adui,
Usinikomoe mimi, ukajikomoa wewe !
Uerevu kajitia, naye mvaa kikoi,
Na jana hakujijua, wala kuwa nayo rai,
Ila leo kajaliwa, mbwa mwitu alo mwui,
Usinikomoe mimi, ukajikomoa wewe !
Kaikoleza tabia, hajifai kwa nikahi,
Uraibu aitia, hata inakuwa hoi,
Kisha kujitapikia, ili hali hajijui,
Usinikomoe mimi, ukajikomoa wewe !
Husuda imemjaa, kitanzi hakiachii,
Mashavu yamemjaa, gubu halimuachii,
Aibua na kuzua, ya watu kutoa uhai,
Usinikomoe mimi, ukajikomoa wewe !
Alalia, aamkia, na sala kaisabahi,
Huku utu ajitia, na shetani amrai,
Mushiriki amekuwa, Afu hamuangalii,
Usinikomoe mimi, ukajikomoa wewe !
Tadi na inda zajaa, wala kwake si jinai,
Moyo kutu waizua, ya ndugu hafurahii,
Si wa kujitambua, kafa ili ayu hai,
Usinikomoe mimi, ukajikomoa wewe !
Akili ameishiwa, hili lile hayajui,
Chombo anakitumia wengine walichokinai,
Na mishipa yamjaa, kwalo hilo kazirai,
Usinikomoe mimi, ukajikomoa wewe !
Kaishia muishiwa, kwa Mumiti na Muhyi,
Ameishaingiliwa, alimoko humtoi,
Ila litamuumbua, vuvuzela likirai,
Usinikomoe mimi, ukajikomoa wewe !
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment