Sunday, November 18, 2012

Aali wastahili



Akili zikifulia, madoho huyaridhia,

Mbali hautoyajua, wala hutojionea,

Yako ukayadhania, ni makubwa yamekuwa,

Aali wastahili, tumeangusha wananchi !



Yetu ukiangalia, sisi nyuma twabakia,

Sote tulipoanzia, sawasawa ilikuwa,

Kundi ukilichukua, twadorora Tanzania,

Aali wastahili, tumeangusha wananchi !



Ni bure kujisifia, kwa ukweli lisokuwa,

Ili wende hurumiwa, wembe ukiandaliwa,

Kinyozi hajajinyoa, naye huomba nyolewa,

Aali wastahili, tumeangusha wananchi !



Ila walioingia, mashine wanatumia,

Hiyo hiyo hutumia, na wao wakajinyoa,

Kisha wakatuzingua, na hasira kututia,

Aali wastahili, tumeangusha wananchi !



Mengine ni kunyamaa, sauti kutotoa,

Chumvi ukizidishia, chakula hakitaliwa,

Kwanza mngeliyajua, uzito kujipimia,

Aali wastahili, tumeangusha wananchi !



Pande mkaangalia, ni wapi imezidia,

Kama kwenu imekua, hayao yenu manufaa,

Wengine huangalia, kama wana manufaa,

Aali wastahili, tumeangusha wananchi !



Kitu wasipoambua, vipi watakusifia,

Mtu bora kujijua, na hadhara kuijua,

Wapo wa kushangilia, kwa malipo kugaiwa,

Aali wastahili, tumeangusha wananchi !





No comments: