Wednesday, November 14, 2012

Ukuu wote huisha


Duniani huishia, mbinguni hautoingia,

Mamlaka umepwa, mwenyewe kuja kufaa,

Vibaya ukitumia, wapi kwenda kuishia ?

Ukuu wote huisha, papa hapa duniani!



Kiumbe usipojijua, Mola ukamtania,

Moja kwa moja haijawa, kwa watuwe hupitia,

Huanza wewe laniwa, hali haujajifia,

Ukuu wote huisha, papa hapa duniani!



Mtihani umepewa, kiumbe hili hofia,

Usivimbishe kifua, kikaja kutobolewa,

Akiridhia Jalia, yako hayawezi kuwa,

Ukuu wote huisha, papa hapa duniani!



Uchamungu wakitia, wa kweli uliokuwa,

Sababu haitakuwa, nje kwenda kutembea,

Palepale wakikaa, kuna dua zaridhiwa,

Ukuu wote huisha, papa hapa duniani!



Kitabu wakikitumia, vizuri ilivyokuwa,

Tajwidi wakajua, na wasiwasi kutoa,

Kwa sababu wanjua, asikia wa kwambiwa,

Ukuu wote huisha, papa hapa duniani!



Huwajua wa dunia, rahisi kununuliwa,

Imani wakabomoa, isilete manufaa,

Kwa sababu ya ukiwa, watu wakimbia njaa,

Ukuu wote huisha, papa hapa duniani!



Huiamini dunia, ndio yenye manufaa,

Na riziki waletewa, si na Mungu bali dunia,

Imani kujizikia, wakabaki wanalia,

Ukuu wote huisha, papa hapa duniani!



Watu kama hao huwa, hawalipwi ya kufaa,

Mzigo huchukuliwa, utumwani kurejea,

Kadhaba ikishakuwa, rehema zinapotea,

Ukuu wote huisha, papa hapa duniani!



Ila kwa wanaojua, kwa Mola watarejea,

Msamaha wakatia, ya kwao kusaidiwa,

Na siku huja fikia, wapendalo ndilo huwa,

Ukuu wote huisha, papa hapa duniani!

No comments: