Wednesday, October 31, 2012

Simama uhesabiwe

Mkono sasa tumia, juu ukaunyanyua,
Wito ukaitikia,  taifa kutumikia,
Uongofu lalia, ni nani wa kulifaa,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Wakati ni huu hawa, wapaswa kuhesabiwa,
Kwa upande kuchagua, kusimama kutetea,
Heri ukiichagua, shari hutolichukua,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Bahari yachafuliwa, na wengi maharamia,
Meli wameidandia, wahofu mabaharia,
Ya heri tukiamua, nahodha tutamfaa,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Nahodha tukimfaa, akili zitatulia,
Meli kujiongozea, hadi nanga tukatia,
Na wengine kuachia, wasoitaka balaa,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Na salama Tanzania, ikazidi kubakia,
Ghasia kuziondoa, za wasya hasiria,
Mabomu kutochimbua, viazi tukidhania,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Rushwa imeshatapakaa, kama panya tumekua,
Paka tunamuhofia, mafichoni twaingia,
Kila anayeisikia sikio ajifumbia,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Nani mwenye ushujaa, mhanga kujitolea,
Kama babu wa India, uzee kajipambua,
Kitalini kaingia, bure wakamzuia,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Kila mtu ashangaa, wakubwa kando kulia,
Ngoma kati imekaa, pembeni waugulia,
Nani aliyetakiwa, ujemadari kuuvaa ?
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Uongo ukitumiwa, mwisho ukweli ukawa,
Nani atatuelewa, timamu waliokuwa,
Guu limetangulia, kule tusikotakiwa,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Musuli waliopewa, kwa kuwatunza hidaya,
Leo wafanya mabaya, hila wanaitumia,
Nyara watu wote kuwa, wapendavyo ndivyo huwa?
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Haitojenga hadaa, nchi safi ilokuwa,
Viinimacho vikiwa, maruerue hujaa,
Turudi nyuma raia, na msokuwa raia,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Kioo tumekikimbia, twezacho jiangalia,
Taasisi zazaliwa, bure hela kutumiwa,
Na kazi zilizopewa, rukusa zakataliwa ?
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Sasa kihoro watia, wakubwa waugulia,
Kucheka najizuia, kila nikiwasikia,
Au yaweza ikawa, tuna 'bosi' tusomjua ?
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Mwenzi ngao augua, kilemba kukikazia,
Kinamama ni bidhaa, leo wananunuliwa ?
Nini kilichobakia, nchi bado kupotea?
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Wazee kwa yao njaa, waukubali udhia,
Nani wa kuwaangalia, wasiende nunuliwa,
Hali ilivyo ni mbaya, kapuni wataingia,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Vijana tunawagawa, kwa fefha kuwarushia.
Huku tunachekelea, wanavyozipigania,
Masalale naitoa, Mola kutuhurumia,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Wazazi gumba wakiwa, huko huko  twelekea,
Ndoano kuiachia, kazi kubwa itakuwa,
Yao yote wamefulia, nin kilichobakia ?
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Watu wanaulizia, hivi hii ndiyo njia,
Nyerere katuachia, sisi kuifatilia,
Au tumeshapotea, twanda tusikokujua ?
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Mishipa imetujaa, twazidi kung'ang'ania,
Twajua tumekosea, tayari twakoselewa,
Kukubali twaktaa, sawa tunajionea,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Sasa waliojaliwa, katikati waingia,
Samaki wanawavua, nchi kavu walokuwa,
Mipango tumefulia, baharini kwenda vua,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Mipesa waitumia, vijana kuwanunua,
Kisha pande tukagawa, hawa na wasiokuwa,
Kule macho twafumbia, huku twawakolea ?
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Dabo standadi mbaya, mbali hatutafikia,
Basi tulilodandia, tairi zajichimbua,
Bondeni twaelekea, na kingo kusikokuwa,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Mamlaka zatakiwa, haki kuisimamia,
Vingine inapokuwa, kadhia naihofia,
Utu waja kujifia, Tanzania italia,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Kiooni kujangalia, muda umeshawadia,
Tena bila kuchelewa, tusije kuadhiriwa,
Tutofautishe ubaya, na mazuri kuchagua,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Huu ni wangu usia, moyoni ninautoa,
Nchi hii kwangu ua, waridi lilotulia,
Kwa amani na umoya, bara linajipambia,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Watu wangu wema huwa, ila wanapoonewa,
Kisha wakabaguliwa, kufanzwa kisichokuwa,
Moyoni wakiumia, mateke wataachia,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Walojuu watakiwa, haki kuisimamia,
Kuna vyombo vyaingia, haki sasa zinaua,
Macho mkiyafungua, ukweli mtautambua,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Naasa kutoamua, pasina kweli kujua,
Daudi alitubia, kosa alipotambua,
Vingine ikijakuwa, ujibari ni nazaa,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Mola nakugeukia, Maulana ulokuwa,
Mtukufu na mjua, njia unazawadia,
Sahihi iliyokuwa, watuwe kutopotea,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!

Nasi twakuangukia, mustakimu kuijua,
Taifa kusaidia, salama likabakia,
Vizazi vikafatia, bila ya kuhujumiwa,
Simama uhesabiwe, nchi ilipokutaka!







No comments: