Sunday, October 7, 2012

Rais asiwe Mungu



Katiba ukichambua, na yeye pia raia,
Na mizani yakataa, uzito ukizidia,
Yetu hutuharibia, pasiwe pa kulilia,
Rais asiwe Mungu, Afrika twakosea!

Huyu mkubwa raia, umungu hajafikia,
Ukweli akijaliwa, heshima kumgawia,
Uongo akitumia, moyoni ni kumtoa,
Rais asiwe Mungu, Afrika twakosea!

Na asipotuibia, sisi tutamuangalia,
Uwizi akijaliwa, kibaka kwetu akawa,
Sheria ikafatia, na dharura kufanzia,
Rais asiwe Mungu, Afrika twakosea!

Umoja akiuua, kwa makundi kuyazua,
Ili yake kumfaa, na yetu tukafulia,
Kiti tukimuachia, wenyewe tutakosea,
Rais asiwe Mungu, Afrika twakosea!

Katiba akichengua, na vikwazo kuvitia,
Akazipika sheria, majaji wapishi kuwa,
Huyo kumvumilia, hivi sawa itakuwa?
Rais asiwe Mungu, Afrika twakosea!

Dola akiitumia, kuwanyanyasa raia,
Ni makosa ayazua, heshima tutaondoa,
Na pembeni kumwambia, kwa hiari ngazi kuachia,
Rais asiwe Mungu, Afrika twakosea!

Taifa huendelea, japo watu twajifia,
Hakuna juu wa kuwa, hata rais akiwa,
Usawa kutengenea, ndio salama twaambua,
Rais asiwe Mungu, Afrika twakosea!

Binadamu wangekuwa, hawautungi ubaya,
Wachamungu tukapewa, madhambi wasiokuwa,
Ndio ingelifaa, kama huyo naye kuwa,
Rais asiwe Mungu, Afrika twakosea!

Twayaona Tanzania, Nyerere kutangulia,
Mengi ametuachia, mazuri yaliyokuwa,
Ila wanaofatia, mabaya wayachagua,
Rais asiwe Mungu, Afrika twakosea!

No comments: