Sunday, October 7, 2012

Polisi wake Nyerere

Walikuwa watu wema, kama ni ndugu twaishi,
Hakuna jogoo mwitu, aliyejaribu uzushi,
Mzee alikuwa wetu, karibu nasi kaishi,
Hivi wameondoka naye, polisi wake Nyerere?

Tumeizusha dhuluma, na vingine hatarishi,
Wanazipika hujuma,  na mdomoni ucheshi,
Lakini kuna tuhuma, wanazishika beleshi,
Hivi wameondoka naye, polisi wake Nyerere?

Watumikia uchama, hata kwa yetu mazishi,
Ni bure tukilalama, bila kwayo hawaishi,
Hadi pawe na cho chama,  kinachojua utashi,
Hivi wameondoka naye, polisi wake Nyerere?

Bure wanatusakama, hali tunataka kuishi
Daima wanalalama, upinzani na ushashi,
Waogopa kusakamwa, uchafu na ushawishi,
Hivi wameondoka naye, polisi wake Nyerere?

Hili sioni alama, ya kuepuka mazishi,
Watu wataka hekima, si ukushi na urushi,
Sana watakutazama,  na kinyongo hakiishi,
Hivi wameondoka naye, polisi wake Nyerere?

No comments: