Wednesday, October 31, 2012

Bado kujitegemea




NANI amekuambia, doa kujitegemea,
Uongo ninakwambia, hiyo ni kubwa nazaa,
Hakika ya ujamaa, jambo hili ulijua,
Falsafa yatufaa, watu kujitegmea.

Komunisti si ujaamaa, tunapaswa kuelewa,
Wakiafrika ulikuwa, ni kuishi kijamaa,
Katika hilo tambua, ukwasi haujazuiwa,
Falsafa yatufaa, nchi kujitegmea.

Ila kinachotakiwa, sera zake kuandaa,
Pasiwe wa kufa njaa, watu wakachekelea,
Sasa inavyokuwa, ushindani twajionea,
Falsafa yatufaa, watu kujitegmea.

Washindana wajaliwa, na kucheka wasokuwa,
Mbio zingine udhia, za magari kununua,
Na majengo kuinua, mtu asikojikalia,
Falsafa yatufaa, nchi kujitegmea.

Israfu tunatia, na baraka kuengua,
Kiburi kimetujaa, na jeuri twatumia,
Hili halina ridhaa, adhabu naihofia,
Falsafa yatufaa, watu kujitegmea.

Demokrasi-jamaa, ndiyo inayotufaa,
Utajiri kuridhia, kwa umoja na wingi pia,
Ila tukayakataa, watu wetu kufa njaa,
Falsafa yatufaa, nchi kujitegmea.

Na mifumo kuibua, udhibiti maridhia,
Na miundo kuandaa, haki inayoridhia,
Kupata kutouziwa, na kukosa kuzuia,
Falsafa yatufaa, watu kujitegmea.

Watu wote twatakiwa, kwanza nyumba kupatia,
Inayofata hatua, fedha za kuwezeshea,
Kila mtu kuvumbua, lake la kujifanya,
Falsafa yatufaa, nchi kujitegmea.

Serikali yatakiwa, wajuzi kuwatumia,
Masoko kuyatambua. popote yalipokaa,
Na nini chatakiwa, jamii kuzalishia,
Falsafa yatufaa, watu kujitegmea.

Miaka imefikia, vitu kujitengezea,
Ni aibu kununua, trekta la Asia,
Amerika na Ulaya, watazidi kutwonea,
Falsafa yatufaa, nchi kujitegmea.

Mitambo ni kuamua, wenyewe kujiundia,
Nje tukitegemea, watakuja tuumbua,
Tuwe tunafikiria, kama vikwazo twawekewa,
Falsafa yatufaa, watu kujitegmea.

Bado kujitegemea, kubwa nuni Tanzania,
Hili tukizingatia, shuleni itarejea,
Na ada zikapungua, kwa jasho letu kutoa,
Falsafa yatufaa, nchi kujitegmea.


No comments: