Sunday, October 7, 2012

Tulijizika wenyewe



Wao tulinyenyekea, kwa vizawadi kupewa,
Baadhi mungu wakawa, wapaswa kuabudiwa,
Kumbe wana yao nia, na sasa inatimia,
Tulijizika wenyewe, sasa na tujifufue !

Waandishi mwatakiwa, sikuzote juu kuwa,
Mkatae kununuliwa, na wakubwa kutumiwa,
Mizizi mkaitia, nguzo ya nne kukomaa,
Tulijizika wenyewe, sasa na tujifufue !

Akili mkitumia, ajira inawafaa,
Mbili, tatu kufatia, ukiritimba kuvia,
Haki mkasimamia, kazi mliochaguliwa,
Tulijizika wenyewe, sasa na tujifufue !

Wanangu niliwambia, pabaya mnaingia,
Watu walipowajia, magari bure kupewa,
Na vyeo kuahidiwa, ukuu mtapatiwa,
Tulijizika wenyewe, sasa na tujifufue !

Hakuna wa kusikia, kama vichaa mkawa,
Mambo mkaparamia, na utu mkajivua,
Miaka naangalia, balaa nikingojea,
Tulijizika wenyewe, sasa na tujifufue !

Mwanzo yanapoanzia, kwa wengine yatakuwa,
Ila alama nazijua, wakati ukifikia,
Utamu ukishakolea, budi kuwageukia,
Tulijizika wenyewe, sasa na tujifufue !

Waandishi mwatakiwa, hadhi yenu kunyanyua,
Shamba la kuaminiwa, robo nne mnakuwa,
Zima hatutofanikiwa, bila nafasi kutwaa,
Tulijizika wenyewe, sasa na tujifufue !

Miradi mnatakiwa, hivi sasa kuizua,
Kipato chenu kukua, fisadi kutotegemea,
Wito kwenu nautoa, kazi niyewaachia,
Tulijizika wenyewe, sasa na tujifufue !

Ushauri nitatoa, tena bure nawambia,
Chama chenu kufufua, cha wote kilichokuwa,
Haki zenu kutetea, nchi isijepotea,
Tulijizika wenyewe, sasa na tujifufue !

TUJ kuazimia, lazima kuifufua,
Na mvi tuliokuwa, twaweza isimamia,
Maoofisini kwingia, na saini mkatia,
Tulijizika wenyewe, sasa na tujifufue !

Wamoja msipokuwa, iweje Watanznia,
Kwanza mngeanzia, na wengine kufatia,
Na swahiba wanasheria, ushauri wakatoa,
Tulijizika wenyewe, sasa na tujifufue !

Nyakati ninahofia, mageuzi yaingia,
Na wapo wenye vichaa, watataka kuzuia,
Upepo unaokimbia, kwa maguvu kutumia,
Tulijizika wenyewe, sasa na tujifufue !

Mola ninawaombea, ya kwenu kufanikiwa,
Mwangosi namtakia. peponi kukubaliwa,
Nyuma tuliobakia, mhanga kajitolea,
Tulijizika wenyewe, sasa na tujifufue !

Manani nakuangukia, waja kuwaangalia,
Kuijenga Tasnia, salama iwe Tanznia,
Uafrika ni dawa, ugeni kuuchukia,
Tulijizika wenyewe, sasa na tujifufue !


No comments: