Saturday, October 13, 2012

CCM 2012




Hii leo itakuwa, tarehe inafikia,
Kumi na tatu tarihia, na miaka kesho pia,
Kumbukumbu kuitia, na bora kudadavua,
CCM ilishaaga, hii ya leo si ya jana !

Kuna kundi lanuia, uoza kzungushia,
Juu huko lakotea, na mema kusikokuwa,
Mikosi inakotokea, nuksani na balaa,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Waua demkrasia, ndiko wanakotokea,
Chama kinawavumilia, na yao kuyasikia,
Walitoa wanatwaa, kama walivyonuia,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Uoza tuliachia, ndani ukajitandia,
Baba alipotwachia, hii ya sasa kadhia,
Wajumbe kununuliwa, na mifuko walojaa,
CCM ilishaaga, hii ya leo si ya jana !

Chama sasa kimekua, ni kinara wa rushuwa,
Kwa huko kweza ingia, nchi nzima kuenea,
Wenyewe tunalilea, bomu la kujilipua,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Fisadi tunawajua, ni swahiba wamekuwa,
Mwalimu atulilia, sisi tunashangilia ?
Kadhaa ya kutapeliwa, na nchi wanaonunua,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Hao wanaonunua, nao wameshanunuliwa,
Na bei yaoghofya, masikini wenye njaa,
Kiazi utadhania, wala ndizi haijawa,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Ganzi imeshatiwa, na nyenzo waliotoa,
Kadhia kutapeliwa, na viranja wenye njaa,
Mikoa wainunua, shibe ilikopotea,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Chama tukakiachia, hasidi kukichukua,
Wapendao kuchafua, na wengine kufagia,
Matope wamekitia, na tope tunaogea,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Hii si ilyokuwa, hiki ni kitu kipya,
Kama ktu chazaliwa, kipo kilichojifia,
Na zamani nagundua, uhai kishautoa,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Kama kufa inshakuwa, yabaki kufufuliwa,
Ibra nazingatia, vigumu haitakuwa,
Ila pawe nayo nia, ukweli kutangulia,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?
Chama kimenipotea, mimi kilichonilea,
Na shuleni kunitia, bure nikajisomea,
Yatima sikuachiwa, mtaani kuteketea,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Chama nimekiachia, asili wasiojua,
Sasa wakichakachua, sio kile kimekuwa,
Hiki kabisa kipya, nami ninakikataa,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Yusiligi nilikua, katibu kutumikia,
Msingi nilipokuwa, asili ninaijua,
Moshi -Arusha najua, kwa mguu nilitembea,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Moshi-Arusha tambua, kwa mguu niltembea,
Azimio kusifia, na Mwalimu kumjua,
Kauli ninayojua, si hiki kilichokuwa,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Kauli sio sawia, wenzetu wanazotoa,
Watumia kusikia, washindwa kujionea,
Taifa linaugua, chama chetu kuugua,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Nani angetumia, fedha kujipalilia,
Mwalimu akamwachia, chamani akaingia,
Kinyume imeshakua, wapendwa wenye kujaa,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Wadhibiti watakiwa, chama kuja kichungua,
Ukweli tukaujua, na pumba kuziachia,
Na nje wakitokea, bora sana itakuwa,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Wachawi wakawajua, walozi waliokuwa,
Wanaotuharibia, chama kilichojaliwa,
Na kukifanya udhia, watu wakakichukia,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Hivi vipi inakuwa, wachache kukubalia,
Chama kutuharibia, na jina kulichafua,
Ushindi ukapotea, kwa uoza kung'ang'ania?
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Au wawe ni jamaa, toka kwenye familia,
Udugu unatitia, magugu yanaingia,
Kama vile wafulia, mengine  kuyasomea,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Muda nimevumilia, ila sasa nayatoa,
Ndani wanaojitambua, chama waje kuokoa,
Njia kimeshapotea, na bado kinaendelea?
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Siasa ninayojua, chama bora huchukua,
Watu wake huchagua, kama mchele ikawa,
Jiwe kutokubakia, kwa hadhari kuondoa,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Kelele tumechagua, si busara twatumia,
Vishindo tunavijua, mikakati yapungua,
Na vijiji vyaugua, ngome ya kutegemewa?
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Ya juu twaangalia, ya chini yanazolewa?
Na wajanja tumezaa, kweupe watuhadaa,
Sherehe wazitumia, uchafu kuufagia!
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Nendeni kwenye mitaa, watu mkawasikia,
Vijana wa Tanzania, na wazazi wao pia,
Lawama wanazotoa, salama haitakuwa,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Tabaka tumeibua, na zinazidi kukua,
Kuna watu watumia, milioni kulelea,
Hali wengi wamejaa, mia inawakimbia,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Ghorofa tunapaua, nyasi zinaendelea,
Vijiji vinafulia, vyabakia kuogelea,
Matope wanajinywea, eti tumeendelea?
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Wengi ninawashangaa, giza kulalamikia,
Kuna Watanzania, taa wasiozijua,
Vijinga wanatumia, na moto wa kukokea,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Kuna watu waingia, haramia wanakuwa,
Chama washikilia, wengine wanazuia,
Hodi ukijigongea, mlango hutofunguliwa,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Matawi sasa rejea, taka za kurejelewa,
Kikundi kinachokua, hatamu kutoachia,
Kama kama kinavia, na hasara kinakuwa,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Ushirikina wazua, watu ghafla kwugua,
Wengine wanajifia, ofisini wamekaa,
Watu wanakihofia, huku chini kuingia,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Na juu nakuhofia, hadithi moja ikawa,
Imepotea ridhaa, masikini kuondoa,
Mizizi tumeing'oa, muhali mmea kukua,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Hoja zimejiozea, sasa tunazotumia,
Na mbinu zimeshapwaya, mpya zinatakiwa,
Mikakati kuifua, sasa budi itakuwa,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Hiki kizazi kipya, ujanja kitazidia,
Palipochimbiwa si dawa, wao watapafukua,
Kilichofichwa si dia, wao watakifichua,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Na teknohama twavia, tovuti kutotumia,
Matawi yanasinyaa, yaambaa teknolojia,
Wakati umeshawadia, vitu hivi kutumia,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Chama imara kikiwa, ni imara Tanzania,
Kudhoofu tukiachia, watu watatunyanyapaa,
Na hazina imejaa, chama hiki kuokoa,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Sasa kinachotakiwa, ni vizuri kuchagua,
Watendaji nadhania, ni bora kuajiriwa,
Sio kuchaguliwa, ili miaka kukaa,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Hata gani kuchagua, nani atamwagilia,
Wote wanaokimbilia, unafsi tupu wajaa,
Yao wanakimbilia, sio chama kuokoa,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Chama ninachokijua, sio tunachojionea,
Hiki ni chama kipya, kile kilishajifia,
Na kaburini kutiwa, toka Mwinyi kuingia,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Dereva nyuma kakaa, adhani anatembea,
Kumbe kinchotembea, mengine yajipitia,
Siri wameigudnua, hili bovu limekua,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Wanalazimisha ndoa, umoja zisizokuwa,
Kauli ukisikia, amani hutoijua,
Na sasa twajionea, sinema yaendelea,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Walzika ujamaa, kwa zao kubwa tamaa,
Wanyonge wamewatoa, wenye fedha wabakia,
Chama kimeshajiua, kwa viongozi kununuliwa,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Ni jina limebakia, maudhui wameng'oa,
Ubaba umepakuliwa, na ubwabwa kupikia,
Kisha wamefunikia, na udugu kuutia,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Chama kilichowatetea, wanyonge wa Tanzania,
Hamna, kimejifia, rangi tu zinabakia,
Mawaridi na maua, kila rangi kujitia,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Cha tajiri kimekua, watu waliowaibia,
Mafuta wayatumia, mwilini waliyotutoa,
Wenyewe kutukangia, hadi tunaungulia,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Mkuu katuambia, kabla tutajifia,
Amin, twaitikia, mbona walishatangulia,
Wafu wameshabakia, ingawa wanatembea,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Na nyie mnaongojea, jidude kujipasua,
Kugawika hadi kuwa, viwili vimetokea,
Ni ujinga mwatumia, chama kilishajifia,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Gamba tu linabakia, makombo kukimbilia,
Wenye pesa kuachiwa, wazidi kukokotoa,
Uoza inshakuwa, samaki wajiozea,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Kwani hamkulijua, mmoja ukimuachia,
Samaki kujiozea, pakachani kubakia,
Huoza wote pamoya, pasiwe wa kuokoa,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Ndivyo ilivyotokea, fisadi walipobakia,
Magamba wakakataa, kamwe hawataondoa,
Uoza uksambaa, kinanuka Tanzania,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Nani watamchagua, kuoza akakataa,
Uozo sasa ni ndoa, ya Katoliki imekua,
Pete kidole kutia, kuachwa haitatokea,
CCM ilishakufa, kigawike chama gani!

Vijana wanafulia, uoza kuegemea,
Kelele wajipigia, za kwenda kujiozea,
Waamka Tanzania, uoza hawatachagua,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Mwalimu aliwausia, uoza kutochagua,
Na majina wawajua, na vyeo walivyokuwa,
Na tabia ilokuwa, imezidi endelea,
CCM ilishakufa, kigawike chama gani!

Na tabia ilokuwa, imezidi endelea,
Makilla katuambia, toka zamani najua,
Nasi hatukumsikia, na sasa tunajionea!
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Chama wanaongojea, eti kujifaragua,
KIkagawika kwa nia, na shabaha nisojua,
Hilo katu nakataa, leo halitatokea,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Kuna wazungu wa njaa, chakula wanakigawa,
Maana wamedhamiria, ya kwao kuyatungua,
Kwa kutumia majuha, nchini waliojaa,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Ah, nchi yangu yaumia, na chama nakillia,
Ukiwa chaniachia, sina wa kutumainia,
Ndugu na zangu jamaa, sasa tumeondokewa,
CCM ilishakufa, kife tena mara ngapi ?

Haukuwa ujamaa, bali siasa za sawa,
Na hili kulikataa, kitali kimeanzia,
Haki ikishauawa, hubatilika ridhaa,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Haukuwa ujamaa, ila mnyonge kufaa,
Neti ndogo ukitoa, mapapa tu utavua,
Ndilo linalotokea, chamani waliojaa,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Huridhishi yao njaa, ya kuzidi limbikia,
Wataka kujipanua, na kuimega dunia,
Mbio wanazikimbia, za utajiri kutwaa,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Olympiki twafulia, ubepari wa sinzia,
Umma unaoibia, wenyewe ukajifaa,
Pikipoketi twazaa, bila ya kujitambua,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Nchi tumeiachia, mirija inachimbiwa,
Na kupe watapakaa, kwa kushoto na kulia,
Mapenzi waliyojaa, mali asili kutwaa,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Twadhani watujengea, kumbe watubomolea,
Na ulinzi twautoa, waendelee bomoa,
Ni ajabu ilokuwa, utadhani ni ruia,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Atuongoe Jalia, mtu kutotegmea,
Yeye kumgeukia, ndiyo tutafanikiwa,
Vingine ninawaambia, tunaenda kufulia,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Kama Mungu twamchagua, binadamu wa dunia,
Mola hatatukatalia, huyo atatuachia,
Ila vyeka kuchukua, utupu tukabakia,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Mwalimu kanibarikia, mkono kichwani kutia,
Mdogo nilipokuwa, na adhima naijua,
Jinsi nilivyojisikia, na hivi leo nalia,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Huyu tunayemtegemea, aachiwe kutufaa,
Kiumbe ni muishiwa, hata kama bilionea,
Siki haitakawia, Ugiriki kufikia,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Njo'ni msionunuliwa, chama chenu kuokoa,
Mashinani kuanzia, pia zote jumuiya,
Kifo  kweli kitakuwa, hali mnaangalia,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Njooni na mashujaa, ukweli mnaojua,
Chama kukipigania, safu bora kuzizua,
Na kuondoa udhia, aibu nayo kinaya,
CCM ilishakufa, kife tena mara

ngapi ?

Vijana wa Tanzania, hofuni kununuliwa,
Wenyewe mtajiua, mashaka mkaingia,
Na chama cha kuanzia, wenyewe mnakijua,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Kamati zikinunuliwa, na halmashauri nayo pia,
Nini kitakachobakia, kuuzwa kwa Tanzania,
Ni mtego twawekewa, budi sasa kutegua,
CCM ilishakufa, kife tena chama gani?

Mkutano wabakia, mkuu uliokuwa,
Mifuko watachukua, wajumbe kuwanunua,
Tajiri waliokuwa, trilioni wavuna kwa saa,
Matajiri wameua, CCM tuliyoijua!


Ndimi nisiye na baba wala mama,
(Mwana TANU  na CCM ya zamani.)



No comments: